Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Employment and Relations

News

​Waziri Sangu Aipongeza NSSF, Asema Makusanyo ya Michango Yafikia Trilioni 2.72


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Deus Sangu ameupongeza Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa mafanikio ya kuendelea kuongeza idadi ya wanachama na wachangiaji kutoka 849,886 hadi kufikia 1,703,821.

Aidha, ongezeko hilo ni sawa na asilimia 100.48 kuanzia mwezi Machi 2021 hadi Septemba 2025 hatua ambayo inaonesha ukuaji na uimarishaji wa mfuko huo.

Mhe. Deus Sangu amebainisha hayo Desemba 17, 2025 jijini Dodoma wakati wa mwendelezo wa ziara yake ya kutembelea Taasisi zilizo chini ya Ofisi yake, ili kufahamu utekelezaji wa majukumu yao, kuimarisha uhusiano wa kikazi na kutoa maelekezo yatakayoongeza ufanisi, uwajibikaji na tija katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Vile vile, amesema mafanikio mengine ni pamoja na ongezeko la idadi ya Waajiri kutoka 32,073 hadi kufikia 49,060, sawa na ongezeko la asilimia 52.96. Aidha, ongezeko la makusanyo ya michango kwa mwaka yamefikia trilioni 2.72 kutoka trilioni 1.17.

Katika hatua nyingine, Mhe Sangu ametoa rai kwa NSSF kuendelea kufanya kazi kwa weledi, ufanisi na kuongeza kasi ya kusajiri wanachama ili kukidhi matarajio ya Serikali ya awamu ya sita, inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Awali akizungumza, Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Rahma Kisuo amewapongeza NSSF kwa kuwekeza katika matumizi ya jambo litakalosaidia wanachama kupata huduma popote walipo nchini.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba, ameishukuru Serikali ya kwa kuendelea kuweka mazingira wezeshi yanayouwezesha Mfuko kufanya kazi kwa weledi.