FAQ.

Sheria ya kuratibu Ajira za Wageni Na.1 ya mwaka 2015 (The Non-Citizens Employment Regulation Act 2015) inasimamia nini?

Sheria Na.1 ya kuratibu Ajira za Wageni ilipitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,mwezi Machi 2015,kusainiwa na Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,mwezi Mei 2015 na kutangazwa na kuanza kutumika rasmi tarehe 15/09/2015 kupitia gazeti la Serikali Na.406 la mwaka 2015.Lengo la sheria hii ni kudhibiti na kuoanisha mfumo wa kisheria wa Ajira na shughuli nyingine zinazofanywa na Wageni ndani ya Tanzania Bara. Kwa sheria hii,Kamishna wa Kazi,Tanzania Bara ndiye msimamizi wa utekelezaji wa Sheria na inampa fursa ya kuwa Mamlaka moja ya utoaji wa vibali vya Ajira kwa Wageni. Aidha,sheria hii itaimarisha upatikanaji wa Taarifa za soko la ajira nchini,kwa kusaidia kujenga Data ya Ajira adimu zinazohitajika nchini.

JE KUNA AINA NGAPI ZA VIBALI VYA AJIRA

Kuna daraja 5 za vibali vya Ajira kama ifuatavyo: I. Daraja A – kwa Mwekezaji na waliojiajiri II. Daraja B – Kwa Mgeni mwenye taaluma iliyoainishwa ,Mfano,Madaktari,Wafamasia,Wauguzi,Walimu wa masomo ya Sayansi,Maprofesa wa vyuo Vikuu nk. III. Daraja C –Kwa Mgeni mwenye taaluma nyingine. IV. Daraja D – Kwa Mgeni anayeajiriwa au kushughulika katika shughuli zilizosajiliwa za kidini au utoaji msaada. V. Daraja E –Mkimbizi.

Viwango vya kulipia gharama za Vibali mbali mbali zikoje?

Kuna gharama za kulipia ili kupata kibali kulingana na Daraja zilizopo kama ifuatavyo: • Daraja A –Kwa Mwekezeji au aliyejiajiri mwenyewe---Dollar 1000 • Daraja B –Taaluma maalum zilizoidhinishwa chini ya sheria Dollar 500 • Daraja C –Taaluma nyinginezo Dollar 1000 • Daraja D-Aliyeajiriwa na Mashirika ya Dini au hisani Dollar 500 • Daraja E-Mkimbizi ni Bure.

Ni nyaraka zipi zinazohitajika kuambatanisha wakati wa kuwasilisha maombi ya kibali cha Ajira

Katika mchakato wa kuidhinisha kibali cha Ajira,waombaji wanapaswa kuambatanisha nyaraka zifuatazo zitakazoambatana na Ada ya kibali cha ajira: I. Fomu Na.901 iliyojazwa kulingana na maelekezo. II. Maelezo ya majukumu ya kazi. III. Wasifu wa mfanyakazi(CV) IV. Picha 2 za sasa za mwombaji zenye kima cha Paspoti. V. Vyeti vya elimu ya juu. VI. Uthibitisho kutoka Mamlaka husika za Taaluma,kwa kazi iliyoombewa kibali cha ajira.Kwa mfano,Wahasibu na Wakaguzi,Wahandisi,Madaktari wa binadamu,Wauguzi,Walimu,Wakadiriaji majengo nk. VII. Tafsiri ambayo imethibitishwa na Baraza la Kiswahili au Ubalozi,juu ya Vyeti/Nyaraka zilizo katika lugha nyingine mbali ya Kiswahili na Kiingereza. VIII. Nakala ya Paspoti IX. Kibali cha awali cha Ajira(kwa Maombi ya mara ya pili) X. Leseni ya Biashara XI. Namba ya mlipa kodi(TIN) XII. Kodi ya ongezeko la thamani(VAT) XIII. Cheti cha usajili wa kampuni. XIV. Katiba na kanuni za kampuni. XV. Mpango wa urithishaji katika Ajira XVI. Taarifa nyingine atakazohitaji Kamishna wa Kazi N.B Viambatanisho vyote lazima vithibitishwe na Mwanasheria anayetambulika. Ni muhimu kukumbuka mbali ya kibali cha Kazi(Work permit),mwombaji anapaswa kuomba kibali cha Ukaazi(Resident Permit) kutoka Idara ya Uhamiaji. Mchakato wa kupata Kibali cha Ajira,unachukua wastani wa siku 14 kushughulikiwa,mara baada ya kupokea nyaraka husika.

Je Kibali cha Ajira kina ukomo? Na vitu gani vinaweza kusababisha kufutwa kwa kibali

Kibali cha Ajira kitakuwa halali kwa muda wa miezi 24 tangu tarehe ya kutolewa na kwa kuzingatia masharti ya Sheria hii,kinaweza kutolewa mara ya pili na katika hali yoyote,jumla ya kipindi cha uhalali wa kutolewa kwa mara ya kwanza na ya pili hakitazidi miaka 5. Kamishna wa Kazi anaweza kufuta Kibali cha ajira endapo: • Mmiliki wa kibali pasipo kuwa na sababu ya msingi atashindwa kutekeleza masharti yaliyowekwa kwenye kibali. • Mmiliki wa kibali ataacha kujishughulisha na Ajira ambayo iliombewa kibali. • Ikithibitika mmiliki wa kibali alitoa taarifa za uongo wakati wa kuomba kibali.

Sheria Na.6 ya Ajira na Mahusiano Kazini ya 2004 na Sheria Na.7 ya Taasisi za Kazi ilianza kutumika lini? na Madhumuni ya Sheria hii ni nini?

Sheria Na.6 ya Ajira na Mahusiano Kazini na Sheria Na.7 ya Taasisi za Kazi ilianza kutumika tarehe 20/12/2006 na ilitangazwa katika Gazeti la Serikali tarehe 5/01/2007. Madhumuni ya sheria hizi ni: (a) Kukuza uchumi kwa kuongeza Tija na Ufanisi katika uzalishaji sehemu za kazi ,kwa kulinda haki za Wafanyakazi na Waajiri. (b) Kuunda Vyombo vya majadiliano na kutoa nafasi ya majadiliano na kufunga Mikataba ya hali bora sehemu za Kazi. (c) Kuweka utaratibu wa wazi wa utatuzi wa migogoro sehemu za kazi. (d) Kutekeleza kwa ujumla mikataba iliyoridhiwa na nchi yetu kutoka Shirika la kazi duniani.

Walengwa wa Sheria hizi ,Sheria Na 6 ya Ajira na Mahusiano Kazini na Sheria Na 7 ya Taasisi za kazi ni Nani?

Sheria hizi za kazi zinawahusu Wafanyakazi wote walioko katika Sekta binafsi na Watumishi Serikalini,lakini haziwahusu Askari waliopo katika majeshi ya Ulinzi,kwa mfano JWTZ,Polisi,Magereza,JKT na Zimamoto.

Mikataba ya Ajira ni nini? na Sheria Na.6 ya Ajira na Mahusiano kazini inazungumziaje suala hili.?

Kifungu cha 14 cha sheria Na.6 ya Ajira na Mahusiano kazini kimefafanua aina 3 za mikataba halali kama ifuatavyo: • Mkataba usio na muda maalum (Mkataba wa kudumu) • Mkataba wa muda maalum . (kwa Wataalam na kada ya Menejimenti) • Mkataba wa Kazi maalum. Kwa mujibu wa Sheria hii,haitambui Mfanyakazi aitwaye KIBARUA,au mtu aliyeajiriwa kienyeji bila mkataba,na inasisitizwa ajira zote ni kwa mkataba na kinyume chake ni uvunjaji wa sheria.

Je kuna haki na mipaka ya Migomo sehemu za Kazi kwa mujibu wa Sheria?

Sheria Na.6 ya Ajira na Mahusiano Kazini vifungu 75 hadi 85 vimetoa haki ya Wafanyakazi kugoma. Mgomo utakuwa halali iwapo yafuatayo yatazingatiwa:- (a) Mgomo uwe unahusu maslahi(interest). (b) Suala linalosababisha mgomo liwe kwanza limepelekwa kwenye Tume ya Usuluhishi na Uamuzi(CMA) na ziwe zimepita siku 30 bila msuluhishi kufanikiwa kusuluhisha. (c) Mgomo uwe unaongozwa na chama cha Wafanyakazi. (d) Ni lazima Wafanyakazi walio wengi wawe wanaunga mkono mgomo huo baada ya kupiga kura. (e) Na baada ya siku 30 kupita bila msuluhishi kupata suluhu,itatolewa taarifa kwa mwajiri ya saa 48 inayoeleza kusudio la kugoma.

Je Mwajiri anayo haki ya kuwafungia nje(lock out) sehemu ya kazi,Wafanyakazi wake?

Sheria Na 6 ya Ajira na Mahusiano kazini ya mwaka 2004,kifungu cha 82,kifungu kidogo(1) kimetoa haki kwa mwajiri kuwafungia nje (lock out) sehemu ya kazi Wafanyakazi wake. Ufungiaji nje Wafanyakazi utakuwa halali iwapo:- • Ipo sababu ya kimaslahi(Interest). • Mgogoro umefikishwa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) na suluhu imeshindikana baada ya siku 30 kupita. • Baada ya muda wa suluhu kupita siku 30,Mwajiri atatoa taarifa kwa Wafanyakazi ya saa 48 kuhusu kusudio la kuwafungia nje. Iwapo Mwajiri hatafuata utaratibu huu,kitendo cha kuwafungia nje Wafanyakazi kitakuwa ni uvunjaji wa sheria na aweza kuchukuliwa hatua za kisheria pamoja na kuwalipa fidia wafanyakazi,mapato ambayo wangepaswa kupata kama wangekuwa kazini.