News
Waziri Ridhiwani Kikwete Akutana na Wanafunzi Wenye Uhitaji Maalum
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Ridhiwani Kikwete leo Juni 23, 2025, amekutana na wanafunzi wenye uhitaji maalum kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na kusisitiza dhamira ya Serikali kuwahudumia ipasavyo watu wenye ulemavu.
Katika kikao hicho, Mhe. Kikwete alieleza kuwa Wizara yake imejipanga kuhakikisha watu wenye ulemavu wanazifikia fursa za ajira, mikopo ya asilimia 10 ya Halmashauri (ikiwemo 2% kwa watu wenye ulemavu), na kushiriki kwenye asilimia 30 ya manunuzi ya umma kwa makundi maalum.
Amesema Serikali kupitia miradi kama BBT-Kilimo inaendelea kuwajumuisha watu wenye ulemavu, hasa vijana, katika shughuli za uzalishaji na maendeleo. "Mimi Waziri mwenye dhamana, nitahakikisha haki na stahiki za watu wenye ulemavu zinalindwa na kutekelezwa," alisema.
Kwa upande wao, wanafunzi hao wamemshukuru Mhe. Ridhiwani kwa kuwa karibu nao na kusikiliza changamoto na maoni yao.