News
Waziri Ridhiwani Kikwete abainisha mbinu shirikishi za kukabiliana na changamoto ya dawa za kulevya kwa vijana
Serikali ya Awamu ya Sita imejipanga kikamilifu kukabiliana na changamoto ya dawa za kulevya kwa vijana kwa kutumia mbinu shirikishi na endelevu.
Amesema hayo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Ridhiwani Kikwete katika maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kupiga Vita Matumizi ya Dawa za Kulevya yaliyofanyika jijini Dodoma Juni 24, 2025, ambapo amebainisha mikakati hiyo inalenga kuwalinda vijana ambao ndio nguvu kazi ya Taifa.
Ameeleza kuwa, hatua hizo zinajumuisha pia utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Kitaifa wa Kudhibiti Dawa za Kulevya 2022/23–2026/27, ambao umeweka misingi ya kinga ya kijamii, matibabu, upunguzaji wa madhara na marekebisho kwa watumiaji.
Aidha, amesema Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu inatekeleza Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi, Mafunzo ya Stadi za Maisha kwa lengo la kuwasaidia vijana kufanya maamuzi sahihi, kujiepusha na makundi hatarishi na kuwawezesha kujiajiri ili kukua kiuchumi.
Waziri Ridhiwani aliwasisitizia vijana wajenge nidhamu binafsi na wawe mfano wa kuigwa katika jamii kwa kuepuka mazingira hatari kama matumizi ya dawa za kulevya.