Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

WAZIRI MKUU AZINDUA MKAKATI WA KUDHIBITI UKIMWI


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezindua Mkakati wa Nne wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI 2018/19 – 2022/23 ambao unatarajia kupunguza maambukizi mapya ya VVU kwa asilimia 75 ifikapo mwaka 2020 na asilimia 85 ifikapo mwaka 2023. Matokeo mengine yanayotarajiwa kufikiwa kutokana na mkakati huo ni kupungua kwa maambukizi mapya ya VVU miongoni mwa watoto kwa chini ya asilimia 5 ifikapo mwaka 2023 na chini ya asilimia 2 ifikapo mwaka 2030.

Waziri Mkuu amezindua mkakati huo leo (Jumamosi, Desemba 1, 2018) kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani yaliyofanyika Kitaifa jijini Dodoma na kusema kuwa matayarisho yake yamezingatia matokeo ya mapitio ya Mkakati wa Tatu wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI 2013/14 – 2017/18. Amesema mbali na matokeo hayo pia mkakati huo utawezesha kupungua kwa vifo vinavyohusiana na ukimwi kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2020 na asilimia 70 ifikapo mwaka 2023 na kupunguza unyanyapaa na ubaguzi ifikapo 2023 na kuelekea kutokomeza kabisa ifikapo mwaka 2030.

Hata hivyo Waziri Mkuu amesema mkakati huo umewianisha na kupanga programu mbalimbali zinazosaidia mwitikio wa Taifa zikiwemo afua zinazotekelezwa kupitia mpango wa dharura wa Rais wa Marekani wa uKIMWI (PEPFAR). “Pia Mfuko wa Dunia wa kudhibiti UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria (Globa Fund) na jitihada nyingine za makubaliano ya ushirikiano baina ya nchi mbalimbali na ili kupata matokeo mazuri tunapaswa kuimarisha mawasiliano na uratibu miongoni mwa wadau wote sambamba na kufuata na kutekeleza vipaumbele vilivyoainishwa.”

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema maadhimisho hayo husaidia kubaini changamoto, mafanikio na hivyo, kuja na mikakati ya kupambana na maambukizi ya VVU na UKIMWI. “Siku hii hutoa fursa kote Duniani kutafakari kwa mara nyingine kuhusu tulipotoka, tulipo na tunapokwenda katika mapambano ya UKIMWI kwenye jamii zetu.” Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amezungumzia kuhusu faida za kampeni ya FURAHA YANGU aliyoizindua mwezi Juni mwaka huu, ambapo aliagiza mikoa yote kufanya uzinduzi wa kampeni hiyo kwenye ngazi za mikoa na hata wilaya.


Amsematakwimu zinaonesha kuwa wakati wa uzinduzi wa kampeni ya FURAHA YANGU katika mikoa yote nchini jumla ya wananchi 262,114 walijitokeza kupima VVU, wakiwemo wanawake 136,389 na wanaume 125,725. “Natoa wito kwa Mikoa na Wilaya zote kuwa kampeni hii iwe endelevu. Viongozi katika ngazi mbalimbali tuungane kwenye uhamasishaji wa jambo hili kwani vita dhidi ya VVU na UKIMWI inahitaji dhamira ya dhati na tafakuri ya kina katika kujilinda dhidi ya maambukizi mapya.”

Waziri Mkuu amewahakikishia kuwa kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli itaendelea kutekeleza na kuboresha huduma za upimaji wa Virusi Vya UKIMWI, kuzuia maambukizi ya kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, matibabu ya magonjwa nyemelezi na kupiga vita unyanyapaa wa aina zote kwa WAVIU.