Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

WAZIRI MHAGAMA AWAPA HAMASA TUCTA KUANZISHA VIWANDA


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amewataka viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi kuanzisha viwanda ili kuinua uchumi na kuchangia adhma ya Serikali ya kuwa na uchumi wa viwanda.

Ametoa kauli hiyo hii leo Aprili 26, 2019 Jijini Dodoma wakati wa mkutano wake na viongozi hao uliohudhuriwa na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Mkuchika, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo pamoja na Naibu Waziri anayeshughulikia Kazi, Ajira na Vijana Mhe. Anthony Mavunde ili kujadili masuala yanayohusu wafanyakazi nchini.

Waziri mhagama aliwataka viongozi hao kuwa wabunifu kwa kuanziasha viwanda vitakavyowezesha kujikwamua kiuchumi pamoja na kuwajengea uwezo wa kujitegemea na kukuza mapato ya vyama vyao.

“Niwaombe sana muwe na mitazamo chanya katika kuchangia adhma ya Serikali kuwa na uchumi wa viwanda kwa kuanzisha viwanda vitakavyowawezesha kukuza uchumi mfano viwanda vya chaki, mbao na vingine vingi”, alieleza waziri Mhagama

Aidha aliwaeleza umuhimu wa kuanzisha viwanda hivyo ikiwa ni pamoja na kuchangia ukuaji wa uchumi nchini, kusaidia kuboresha maslahi ya wafanyakazi na kuongeza motisha na kutoa fursa za ajira kwa wananchi kwa ujumla.

“Hii leo nimeona niwape changamoto ya kuona umuhimu wa kuwa na viwanda vyenu kwa kuangalia mchango wenu katika jamii na kuendelea kuwa na tija kwa kuzingatia umuhimu wa kuwa na viwanda nchini,” alisisitiza Mhagama

Kwa upande wake rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini Bw. Tumaini Nyamhokya alishukuru mchango wa serikali na maoni yao kwa kuwapa chachu ya kuona umuhimu wa kuwa na viwanda na kuahidi kulifanyika kazi suala hilo.

“Kipekee nimefurahishwa na maoni na mawazo ya serikali hivyo hatuna budi kuanza kulifanyia kazi suala hilo ili kuendelea kuwa na mchango katika ukuaji wa uchumi wa nchi yetu”, alisema Nyamhokya

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Wanawake Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) Bi. Rehema Ludanga alieleza alivyopokea ushauri huo wa serikali na kuona ni namna bora ya kujishirikihsha katika uchumi wa viwanda na kuonesha utayari wa kufanyia kazi suala hilo.

“Binafsi nikiwa kama mwenyekiti Kamati ya Wanawake nimelichukua kwa dhati kabisa na nitajitahidi kulifanyia kazi mapema iwezekanavyo ili wanawake nao waweze kunufaika na fursa hii hasa upande wa sekta ya kilimo,” alieleza Bi. Rehema.