Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

WAZIRI MHAGAMA ATOA MAAGIZO MAZITO UJENZI WA KIWANDA CHA NGOZI KARANGA


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amesema Serikali haijaridhika na kasi ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa kiwanda cha bidhaa za ngozi cha Karanga katika Gereza la Karanga Mkoani Kilimananjaro na kumtaka mkandarasi kuikamlisha kazi hiyo kabla ya tarehe 2 Februari mwaka huu.

Akikagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo jana (Jumatano Januari 15, 2020), Waziri Mhagama alisema hakuna sababu kwa mradi huo unaotekelezwa kwa ubia baina ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na Gereza la Karanga, kutokamilika kwa wakati kwani fedha zote zilizohitajika katika hatua muhimu za mradi huo zimekwishatolewa.

Kwa mujibu wa Waziri Mhagama alisema kiwanda hicho ni miongoni mwa miradi muhimu ya kimkakati iliyopangwa kutekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano, hivyo mkandarasi hana budi kuzingatia masharti ya mkataba uliowekwa ili kuhakikisha kuwa kiwanda hicho kinakamilika kwa wakati na kuweka kuleta tija iliyokusudiwa.

‘’Sijaridhishwa na kasi ya ujenzi wa mradi huu, na nitoe maagizo kwa Jeshi la Magereza linalosimamia ujenzi wa mradi huu kuhakikisha kuwa kunakuwepo na vifaa, vitendea kazi na wataalamu wa kutosha katika maeneo yote ya ujenzi ili kuhakikisha kuwa tarehe 2 Februari mwaka huu mradi huu unakamilika na baadhi ya mashine zinaanza kusimikwa’’ alisema Waziri Mhagama.

Aidha Waziri Mhagama alisema iwapo mradi wa ujenzi innaonekana ni mkubwa, Serikali itawaruhusu wakandarasi mbadala ikiwemo Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Shirika la Mzinga, na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), kuifanya kazi hiyo ili kukamilika kwa wakati na muda uliopangwa kwani Serikali kupitia kiwanda hicho imekusudia kutengeneza ajira na mapato ya fedha za kigeni.

Akifafanua zaidi Waziri Mhagama alisema mwishoni mwa wiki hii Ofisi yake inatarajia kupokea mashine za mradi huo na kuzikagua, hivyo ni wajibu wa mkandarasi wa mradi kuongeza kasi ya ujenzi wa mradi huo kwa kuwa Serikali kupitia PSSSF kwa upande wake imetekeleza wajibu wake kwa kutoa fedha zilizohitajika hadi kufikia hatua iliyopo.

Waziri Mhagama pia alizitaka taasisi zote zinazohusika katika mradi huo ikiwemo PSSSF, Shirika la Maendeleo ya Utafiti wa Viwanda Tanzania (TIRDO) pamoja na Jeshi la Magereza Nchini kusimamia kwa ukamilifu vifungu vya kitaalamu ili kuufanya mradi huo ukamilike kwa wakati, kwani Serikali haipo tayari kulipa fidia ya gharama za usimakaji wa mashine ikisubiri kukamilishwa kwa ujenzi wa kiwanda hicho.

Kwa upande Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Magereza Nchini, Hamis Nkubasi alisema Jeshi hilo limepokea maelekezo yote ya Serikali na imejipanga kuhakikisha kuwa mradi huo unakamilika kwa wakati ili kuweza kufikia malengo yaliyowekwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Hosea Kashimba alisema hadi sasa Ofisi yake imetoa kiasi cha Tsh Milioni 200 zilizotumika kwa ajili ya ununuzi wa malighafi zote muhimu zilizohitajika katika hatua mbalimbali za ujenzi wa mradi huo.

Alisema kuwa Ofisi yake imejipanga kuhakikisha kuwa itatekeleza maelekezo yote yatakayolewa na Serikali na yanayohitajika kwa mkandarasi ili kuhakikisha kuwa mradi huo unakamilika katika muda na wakati uliopangwa kwa mujibu wa Mkataba.