Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

WAZIRI MHAGAMA ATOA MAAGIZO KWA VIONGOZI WA SHAMBA LA KATANI LA HASSAN SISAL ESTATE


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama ametoa maagizo kwa viongozi wa Shamba la Katani la Hassan Sisal Estate kuhakikisha wanatatua migogoro na wafanyakazi pamoja na kusimamia haki zao ipasavyo.


Waziri Mhagama ametoa maagizo hayo wakati wa ziara yake Wilayani Same alipofanya ziara katika Shamba la Hassan Sisal Estate ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa kuhusu masuala ya kazi aliyoyatoa Julai 20, 2019 alipotembelea shamba hilo lililopo Mkoani Kilimanjaro, Wilaya ya Same.

Akizungumza na wafanyakazi pamoja na viongozi wa shamba hilo, alieleza kuwa waajiri wanatakiwa kutekeleza matakwa yote ya Sheria za ajira na mahusiano kazini kwa kuzingatia miongozo na kanuni ambayo inasimamia haki za msingi kwa wafanyakazi.


“Tunataka kuona ninyi kama waajiri mnakuwa na vikao vyenye tija na wafanyakazi katika kuleta suluhu ya masuala mbalimbali ya kazi,” alisema Mhagama

Aliongeza kuwa Kampuni mbili zilizopo katika shamba hilo yaani Unique Consultancy na UPAMI kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wafanyakazi hao, ikiwemo kuwasilisha michango kwa wakati kwenye Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF). Pamoja na hayo alishauri pia kampuni hizo kuwaweka wazi wafanyakazi kuhusu mikataba yao.


“Malalamiko na Manung’uniko ya wafanyakazi ni mengi, mnatakiwa kukaa na kujadili pamoja namna bora ya kutatua matatizo yao yanayojitokeza hususani kwenye mikataba,” alisema Mhagama.

Katika hatua hiyo, Mhe. Mhagama alimuagiza Meneja wa Wakala wa Usalama na Afya Mahala Pa Kazi (OSHA), kufanya kanguzi za mara kwa mara katika shamba hilo na kuangalia kama wafanyakazi wanakabidhiwa vifaa vya kujinginga na madhara kazini (Protective gears) kwa wakati, pamoja na kusimamia zoezi la upimaji afya kwa wafanyakazi hao.


Pia, alitoa maelekezo kwa Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Mkoa wa Kilimanjaro, kukabidhi kadi za uwanachama kwa wafanyakazi wa shamba hilo la Hassan Sisal Estate na kufuatilia uwasilishaji wa michango yao kutoka kwa waajiri wao.

Sambamba na hilo, Waziri Mhagama ametaka Afisa Kazi Mfawidhi wa Mkoa wa Kilimanjaro kutembelea shamba hilo na maeneo mengine mbalimbali katika mkoa huo ili kuelimisha wafanyakazi sheria mbalimbali za kazi na ajira zitakazo wawezesha kutambua haki zao za msingi.


Aidha, Waziri Mhagama alitoa maelekezo juu ya uwepo wa vyama vya wafanyakazi kwenye mashamba yote ya katani yaliyopo nchini, vitakavyosadia kuongeza tija na ufanisi katika shughuli mbalimbali za utendaji kazi.

Pamoja na hayo, Mheshimiwa Mhagama aliwataka viongozi wa shamba hilo kuendelea kusimamia vizuri maslahi ya wafanyakazi wao ili waweze kutekeleza majukumu ya kila siku wanapokuwa katika maeneo yao ya kazi.


Naye, Meneja Mshauri wa Shamba hilo, Bw. Ndekirwa Nnyari aliahidi kufanyia kazi maagizo yote yaliyotolewa ikiwemo kuwa na majadiliano ya mara kwa mara na wafanyakazi kwa itakayowapa munufaa ya pamoja.


Kwa upande wake, Meneja wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Bw. Victor Luvena amesema kuwa watatekeleza maagizo yaliyotolewa na Mheshimiwa Waziri kwa kuchukua hatua za kisheria kwa wale watakaoshindwa kutekeleza.


Pia mmoja wa Wafanyakazi wa Shamba hilo, Bi. Cheshi Juma alisema kuwa ujio wa Waziri na wataalamu alioambatana nao utasaidia kuondoa kero za wafanyakazi na kujenga mahusiano mazuri na waajiri wao.

“Tumehamasika sana kuona Serikali yetu ipo pamoja nasi katika kutetea maslahi ya wafanyakazi na kushughulikia kero tulizokuwa tukikabiliana nazo katika maeneo ya kazi,” alisema Cheshi