Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Waziri Mhagama Akagua Maandalizi Ya Uzinduzi Wa Mbio Za Mwenge Wa Uhuru Mkoani Songwe


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama amefanya ziara na kukagua maandalizi ya uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru zinazotarajiwa kufanyika tarehe 2 Aprili, 2019 Mkoani Songwe.


Akizungumza mara baada ya kupokea taarifa kutoka kwenye kamati ya Maandalizi, Waziri Mhagama alieleza kuridhishwa na hatua za awali za maandalizi na kuipongeza kamati ya Mkoa kwa kusimamia vyema na kuratibu shughuli za maandalizi hayo.


“Niwapongeze kwa hatua hizi mlizofikia katika kuhakikisha shughuli hii ya kitaifa inafana, maana maandalizi bora yataleta heshima kwa Mkoa katika kufanikisha jukumu hilo muhimu, hivyo mzingatie masuala yote ya msingi na kufanya uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru katika Mkoa wa Songwe una kuwa wa kihistoria,” alisema Waziri Mhagama



Aliongeza kuwa, Mbio za Mwenge wa Uhuru zinahistoria kubwa katika Taifa letu, ikiwa ni mwaka wa 55 sasa tunaadhimisha mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa na ni mwaka wa 27 toka kuanzishwa mfumo wa vyama vingi ikiwa ni kielelezo tosha cha kukua kwa demokrasia nchini.

Vilevile ni miaka 20 ya kumbukizi ya Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere hivyo ni vyema vijana wakatambua historia ya Taifa na kujifunza falsafa za Baba wa Taifa kwa kuwa na umoja, mshikamano, uzalendo, kujitolea na zaidi kuchochea maendeleo ya nchi.



“Kupitia shughuli hii ya kitaifa vijana wanapaswa kutumia fursa hiyo kuelewa historia ya Taifa lao pamoja na Mwenge wa Uhuru kama kielelezo muhimu cha Utaifa,” alisisitiza Mhagama

Hata hivyo, Mhe. Mhagama aliusihi uongozi wa Mkoa kutumia nafasi hiyo kutangaza vivutio vya utalii, fursa za kiuchumi na shughuli mbalimbali zilizopo ndani ya mkoa wa Songwe. Pia aliwataka waendelee kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya uzinduzi.


Naye, Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brigedia Jenerali (Mst.), Nicodemus Mwangela, alipokea maelezo yaliyotolewa na kuahidi kusimamia shughuli zote za maandalizi kwa ufanisi na kukamilisha ndani ya muda uliopangwa.



“Nikuhakikishie maandalizi yataendelea kwa kasi na yatakamilika kwa wakati ili kuwawezesha wananchi wa Mkoa wa Songwe wanashiriki katika tukio hilo muhimu na kuitumia fursa hiyo ya Uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kujitangaza kama Mkoa,” alisisitiza Mhe. Mwangela