Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

WADAU WAOMBWA KUJITOKEZA KUSAIDIA MAANDALIZI YA MASHINDANO YA SOKA KWA WENYE ULEMAVU AFRIKA MASHARIKI


Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu imewataka wapenzi na wadau wa soka nchini kushiriki maandalizi ya mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu kwa watu wenye ulemavu Afrika Mashariki (CECAAF) yanayotarajiwa kufanyika nchini Mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 16, 2019 Jijini Dodoma,katika mkutano uliolenga kuitambulisha kamati ya wabunge watano waliojitolea kuhamasisha Watanzania,kushiriki kwa hali na mali katika mashindano hayo, Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe, amesema kuwa mashindano hayo yatashirikisha nchi za Tanzania Bara, Zanzibar, Uganda, Kenya na Rwanda.

“Mashindano haya yatakayokuwa ya kwanza kufanyika katika ukanda huu wa Afrika yameanzishwa kwa mujibu wa mkataba wa Umoja wa Mataifa wa haki za Walemavu wa mwaka 2006, unaotaka haki ya Walemavu kushiriki katika mambo kadhaa ikiwemo michezo”

Akifafanua zaidi, Dkt. Mwakyembe amesema kuwa lengo la kuhamasisha umma wa watanzania ni kuunga mkono mashindano hayo kwa hali na mali.

Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Waziri mkuu anayeshughulikia watu wenye ulemavu Mhe. Stella Ikupa amesema kuwa mashindano hayo yatasaidia kuibua vipaji vya watu wenye ulemavu na hivyo kushiriki katika kukuza sekta ya michezo.

Pia ameiomba jamii kwa upana kujitokeza kuchangia na kushiriki mashindano hayo kwa kuzingatia kuwa watu wenye ulemavu wana nia ya kushiriki vyema katika mashindano hayo.

Naye mbunge wa Sengerema mhe. William Ngeleja,ambaye pia ni mwenyekiti wa klabu ya michezo ya Bunge, akizungumza kwa niaba ya Spika wa Bunge, amesema kuwa watashiriki kikamilifu katika kuhakikisha kuwa mashindano hayo yanafanikiwa kwa kuzingatia malengo yake.

Mheshimiwa Ngeleja,aliongeza kusema kuwa watashiriki kwa vitendo kwa kuzingatia kuwa Bunge ni wasimamizi wa sheria za sekta ya michezo ,mikataba ya kimataifa, sheria na kanuni katika sekta hii.

Wizara ya Habari kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, inawaomba wananchi kuipa Kamati hii ya wabunge ushirikiano wakutosha katika maandalizi ya michuano hiyo ambayo inahitaji fedha ya kutosha na vifaa.

Wabunge wanaounda kamati hiyo ni Mheshimiwa William Ngeleja,Mheshimiwa Venance Mwamoto,Mheshimiwa Margareth Sitta, Mheshimiwa Amina Mollel na Mheshimiwa Riziki Said Lulida.