News
Wachimbaji Wadogo wa Madini Chunya Wapongeza Serikali kwa Mafunzo ya Kukuza Ujuzi
Wachimbaji wadogo wa madini wa Chunya wameeleza shukrani zao kwa Serikali kwa kuwawezesha mafunzo maalum ya ukuzaji ujuzi, wakisema hatua hiyo ni chachu ya kuwajengea uwezo wa kitaalamu na kuboresha tija katika shughuli zao.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti Wachimbaji hao wa Madini leo Julai 9, 2025 Mwenyekiti mstaafu wa Mberema Mkoa wa Mbeya Bw. Leonard Manyesha, ameshukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia mafunzo hayo ambayo yamekuwa na tija katika shughuli zao za uchimbaji.
Ameongeza kuwa mada walizofundishwa zimekuwa chachu kwa wachimbaji katika kuongeza thamani ya madini.
Naye, Mediko Mbogela, ambaye ni Mchimbaji wa Madini amesema kuwa mafunzo hayo yameongeza uwezo kwa wachimabaji wa madini kuongeza thamani ya madini nakuyabadilisha kuwa bidhaa jambo ambalo litaongeza kipato kwa wachimbaji wadogo.
Aidha, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu imeendelea kutoa mafunzo ya kuongeza ujuzi kupitia Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi kwa kushirikiana na wadau wa Sekta ya Madini ikiwemo Wizara ya Madini, Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), na TGC.
Mada zilizowasilishwa katika mafunzo hayo ni pamoja na mada ya Utafiti na Uchimbaji wa Madini, Uchenjuaji wa Madini, Utunzaji wa Kumbukumbu , Matumizi Salama ya Vilipuzi Migodini na Afya na Usalama Migodini, Uongezaji Tahamani Madini na Utunzaji wa Mazingira Migodini.