Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Vijana Nchini Kuendelea Kuwezeshwa ili Wajiajiri na Kuzalisha Ajira


Serikali imesema itaendelea kutekeleza kwa vitendo azma yake ya kuwezesha vijana hapa nchini ili kuondokana na changamoto ya ajira na kupanua wigo wa ukuzaji uchumi utakaowezesha ujenzi wa uchumi jumuishi.

Akizungumza wakati wa semina kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria leo Bungeni Jijini Dodoma, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu- Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama amesema kuwa, kuwawezesha vijana ni dhamira ya Serikali ambayo inatekelezwa kwa vitendo kupitia programu mbalimbali ikiwemo mafunzo ya ujuzi wa kilimo kwa kutumia teknolojia ya vitalu nyumba (green house) katika halmashauri zote nchini.

“Tunawajengea uwezo vijana wetu bila kujali kiwango cha elimu ili waweze kushiriki kikamilifu kukuza Sekta ya Kilimo kupitia kilimo cha vitalu nyumba katika halmashauri zao kote nchini na pia waweze kueneza ujuzi huo kwa wenzao,” alisisitiza Waziri Mhagama.

Katika programu hii tunawajengea uwezo vijana kuzalisha kisasa kupitia vitalu nyumba ili tuweze kuondoa changamoto ya ajira kwa vijana na pia kutekeleza azma ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli inayosisitiza katika kuwawezesha vijana aliongeza Waziri Mhagama.

“Serikali inawalenga vijana wote waliohitimu elimu ya juu na wale ambao hawakupata elimu katika mfumo rasmi ili waweze kushiriki kikamilifu katika kukuza Sekta ya Kilimo,” alisisitiza Waziri Mhagama.

Kupitia programu hiyo ya ujenzi wa vitalu nyumba, vijana 100 wananufaika na mafunzo kwa kila Halmashauri ili waweze kuwa chachu ya mageuzi katika Sekta ya Kilimo katika maeneo yao na kueneza ujuzi watakaopata kwa vijana wenzio.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Abdallah Mchengelwa amesema kuwa semina kwa wabunge wa kamati hiyo ni nyenzo muhimu katika kuwawezesha kuwa na uelewa mzuri kuhusu mikakati ya Serikali kuwezesha vijana kupitia programu ya vitalu nyumba.

Aliongeza kuwa Teknolojia ya Vitalu Nyumba (Green House Technology) inawezesha vijana kuwa na uzalishaji wenye tija na itawawezesha kuongezeka kwa kiwango cha mazao ya kilimo ambayo yanahitajika katika viwanda kama malighafi.

Pia alitoa wito kwa Serikali kutangaza programu hiyo ya kuwawezesha vijana kupitia mpango wa ujenzi wa vitalu nyumba katika halmashauri zote ili wananchi wengi zaidi wanufaike na matokeo ya dhamira hiyo njema ya Serikali katika kuwezesha kundi hilo ambalo ni nguvu kazi ya Taifa.

Naye Mkurugenzi wa Ajira kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Bw. Ally Msacky amesema kuwa ujenzi wa uchumi wa viwanda unaenda sambamba na ongezeko la uhitaji wa malighafi viwandani.

Aliongeza kuwa kutokana na azma hiyo kwa sasa mkazo umewekwa katika kuzalisha nguvu kazi yenye ujuzi unaoendana na mahitaji ya sasa na mipango ya Serikali ya Awamu ya Tano ili kuchochea ukuaji wa uchumi jumuishi.

Akiwasilisha mada katika mafunzo hayo Meneja Uendeshaji wa Ushirika wa Vijana waliohitimu Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUGECO), Bw. Joseph Massimba amesema kuwa wamejenga vitalu 13 kati ya 14 vilivyopangwa kulingana na mkataba kati yao na Ofisi ya Waziri Mkuu.

“Vijana zaidi ya 280 wamepewa mafunzo ya kuwajengea uwezo na mafunzo haya kwa vitendo yanaleta matokeo makubwa katika uzalishaji kupitia vitalu nyumba,“ alisisitiza Massimba.

Programu ya Ujenzi wa Vitalu Nyumba inatekelezwa kupitia Ushirika wa Vijana waliohitimu Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine ambao wamepewa jukumu la kujenga uwezo kwa vijana wengine katika Halmashauri hizo ambapo wanufaika katika kila Halmashauri ni Vijana 100. Kwa sasa halmashauri za mikoa ya Lindi na Mtwara, wameshanufaika na programu hii inayotekelezwa nchi nzima kwa lengo la kuwakwamua vijana kiuchumi.