Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

SERIKALI KUWAJENGEA UWEZO VIJANA WA MIKOA YA KUSINI KATIKA KUONGEZA THAMANI YA MAZAO YA MBOGAMBOGA NA KOROSHO


Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mhe. Rais, Dkt. John Pombe Magufuli imeandaa mkakati wa kuwajengea uwezo Vijana wa mikoa ya kusini mwa Tanzania wa kuongeza thamani ya mazao ya mboga mboga kupitia programu ya Kitalu nyumba inayosimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu sambamba na kushiriki katika uchumi wa zao la korosho kwa kupatiwa nyenzo za ubanguaji korosho kupitia vikundi vya maendeleo ta Vijana.

Hayo yamesemwa leo na Mh Anthony Mavunde-Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu(Kazi,Vijana na Ajira) kwa nyakati tofauti wakati akikagua vitalu nyumba vya mazao ya mbogamboga vilivyopo katika Manispaa ya Lindi na Wilaya ya Nachingwea Mkoani Lindi.

“Kupitia Mifuko ya Uwezeshwaji wananchi kiuchumi,Vijana watawezeshwa kuweza kuchakata mazao haya ya mboga mboga kwa kupatiwa mashine ndogo ndogo kupitia SIDO.Pia tunatarajia kutengeneza nafasi zaidi za Ajira kupitia zao la Korosho kwa kuwawezesha Vijana mashine za ubanguaji wa korosho kupitia mikopo ya vikundi vya Vijana”Alisema Mavunde

Naye Mbunge wa Jimbo la Nachingwea Mh Hassan Masala ameishukuru Serikali kwa kuwawezesha Mafunzo ya Kitalu nyumba(Greenhouse) Vijana wa Kijiji cha Mwananyamala,Kata ya Luponda-Nachingwea ambapo kupitia programu hiyo Vijana wengi watajiajiri na hivyo kupunguza tatizo la ukosefu wa Ajira.

Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea Mh Rukia Muwango ameishukuru pia Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kutekeleza mradi huu wenye lengo wa kubadilisha vijana fikra na mtazamo juu ya umuhimu wa sekta ya Uchumi katika kujenga uchumi,na kuahidi kwa niaba ya Serikali ya wilaya kusimamia kwa dhati kila hatua ya utekelezaji wa mradi ili tija ionekane na mwisho wa siku kutimiza azma ya kutatua changamoto ya Ajira kwa Vijana.