Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

SERIKALI KUENDELEA KUIMARISHA UPATIKANAJI WA MAJI SAFI NA SALAMA NCHINI


Serikali imedhamiria kuimarisha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi waishio mijini kufikia asilimia 95 na vijijini asilimia 85 ifikapo 2020.

Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mama Samia Hassan Suluhu wakati wa uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Aprili 2, 2019 zilizofanyika uwanja wa Kimondo – Forest Mlowo, Wilaya ya Mbozi, Mkoani Songwe.

Kauli mbiu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu 2019 isemayo “Maji ni Haki ya kila Mtu, Tutunze Vyanzo Vyake na Tukumbuke Kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa”

Makamu wa Rais amesema kuwa dhamira ya Serikali inayoongozwa na Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ni kuboresha huduma za jamii ikiwemo sekta ya elimu, afya, barabara, umeme vijijini, usafiri wa anga, uvuvi, kilimo, viwanda na upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wote.

“Sera yetu ya Maji ya mwaka 2002 inasisitiza upatikanaji wa maji safi na salama ambayo ni muhimu kwa maisha ya kila mtu, shughuli za kiuchumi na ustawi wa mazingira,” alisema Makamu wa Rais.

Akizungumzia kuhusu upatikanaji wa maji safi, alieleza kuwa Serikali inaendelea kutekeleza ujenzi wa miradi mbalimbali ya maji nchini ikiwemo mabwawa ya kimkakati na kuboresha miundombinu ya uzalishaji na usambazaji maji safi.

Aidha, Makamu wa Rais alitoa wito kwa Wananchi kuhakikisha wanatunza vyanzo vya maji kwa kuacha kufanya shughuli za kibinadamu kando ya vyanzo hivyo.

Kupitia hadhara ya Uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Makamu wa Rais, amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi na kushiriki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambao ni muhimu katika kuleta maendeleo ya watu na huduma za kijamii.

Awali Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama alisema kuwa Mwenge wa Uhuru ndio msingi mkubwa wa amani, Mshikamano, Uzalendo na Umoja tulionao katika Taifa.

“Tunu hii imekuwa ni kichocheo cha maendeleo kwa wananchi na wamekuwa wakihamasika kushiriki katika kuandaa na kutekeleza miradi mbalimbali ya kimaendeleo ikiwemo ya kijamii na kiuchumi iliyopo katika maeneo yao,” alisema Mhagama.

Waziri Mhagama aliongeza kwa kuwashukuru wadau mbalimbali waliosaidia kufanikisha tukio hilo muhimu la Kitaifa.

Kwa Upande wake Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Brigedia Jenerali (Mst.), Nicodemus Mwangela alishukuru Serikali kwa kuchagua Mkoa wa Songwe kuwa wenyeji wa Uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa kwa mwaka 2019.