Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Serikali imeendelea kutoa kipaumbele kwa kundi la Wasioona na wenye Ulemavu


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita imeendelea kutambua na kutoa kipaumbele kwa kundi la Wasioona na Watu wenye Ulemavu kwa kutengeneza, kuzindua na kusambaza Mfumo wa Kielektroniki wa taarifa na kanzidata kwa Watu wenye Ulemavu (PD-MIS).

Aidha, Mfumo huo umewezesha kuwatambua, kuwasajili, kubainisha mahitaji yao na kuwaunganisha na huduma za afya, elimu, mafunzo ya ufundi stadi, vifaa saidizi, vyeti vya kuzaliwa na fursa za uwezeshaji kiuchimi ikiwemo Mradi wa Kilimo wa Jenga kesho yako iliyobora (BBT).

Amebainisha hayo leo Oktoba 25, 2024 Mkoani Kilimanjaro, Manisapaa ya Moshi katika Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Fimbo Nyeupe na Miaka 60 ya Chama cha Wasioona Tanzania (TLB).

Mhe. Kassim Majaliwa amesema Serikali imeimarisha miundombinu ya elimu ili kuongeza udahili wa Wanafunzi wenye Ulemavu wakiwemo wasioona na kuhakikisha wanapata elimu iliyobora kwa kununua vifaa saidizi, ambapo kwa mwaka wa fedha 2023/24 Wanafunzi wasioona na wenye uoni hafifu wamepewa vifaa vyenye thamani ya shilingi bilioni 1.36.

Vile vile, amesema Serikali imewezesha kupatikana kwa Mradi wa miaka mitatu mahususi kwa Watoto wasioona na viziwi wenye thamani ya shilingi bilioni 8.2 na Mradi huo unaanza kutelezwa Novemba 2024, hivyo zaidi ya Watoto 300,000 wenye changamoto za uoni watanufaika na mradi huo kwa kupimwa na wataobainika watapewa vifaa saidizi bila malipo.

Awali akizungumza Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Nurdin Babu, amesema amempongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za miradi ya maendeleo ikiwemo za watu wenye Ulemavu.

Naye, Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Wasioona (TLB) Lomitu Lowata amesema Chama cha hicho kinatambua mchango unaotolewa na Serikali kwa kushirikiana na wadau katika kushawishi, kutetea na kuhamasisha upatikanaji wa haki na mahitaji ya Watu Wasioona.