Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

​Rais Samia apongezwa kutoa Bil.9 kuwezesha nguvukazi ya taifa kupata ujuzi


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amepongezwa kwa kutoa Tsh. Bil. 9 kwa kwa Mwaka wa fedha 2024/2025 kwa ajili ya kuwezesha nguvukazi ya Taifa kupata ujuzi stahiki unaoendana na ushindani katika soko la ajira.

Fedha hizo zimetolewa kupitia Programu ya Taifa kukuza ujuzi ambayo imejikita katika mafunzo ya Uanagenzi (Apprenticeshiptraining), Mafunzo ya kurasimisha ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi wa ujuzi, Mafunzo kwa vitendo mahali pa kazi kwa Wahitimu (Internship training) na Mafunzo ya kukuza ujuzi kwa walio makazini.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Ajira na Ukuzaji Ujuzi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Bw. Daudi Silasi wakati wa kufunga mafunzo kwa vitendo kwa wachimbaji wadogo wa madini wa Mkoa wa Geita.

Amesema Serikali imejipanga kuhakikisha wachimbaji wadogo wanakuwa sehemu ya maendeleo ya taifa kwa kuwajengea uwezo endelevu kupitia Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi kwa kuwahusisha kwenye mnyororo mzima wa thamani ya madini.

Akizungumza kwa niaba ya wachimbaji, Bi. Neema John amesema mafunzo hayo yamewasaidia kujitambua kama wadau muhimu katika sekta ya madini na kuwapatia ujuzi utakaowawezesha kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa.

“Tulikuwa tunafanya kazi kwa mazoea bila kujua athari za kiafya wala mazingira. Sasa tunajua umuhimu wa kutumia vifaa sahihi, kuchimba kwa mpangilio na kuhifadhi mazingira kwa manufaa ya kizazi kilichopo na kijacho," amesema.

Naye, Emmanuel Kapunda, amesema mafunzo hayo yamewafungua macho kuhusu fursa zilizopo katika sekta ya madini, hasa kwa wachimbaji wadogo ambao kwa muda mrefu walikuwa wakikumbwa na changamoto ya ukosefu wa elimu ya biashara na usimamizi wa rasilimali.

Mafunzo hayo, yamekuwa yakiendeshwa kwa nadharia na vitendo, yamewajengea uwezo wachimbaji kuhusu mbinu bora za uchimbaji salama, uhifadhi wa mazingira, matumizi ya teknolojia, usalama kazini pamoja na masuala ya kisheria na masoko ya madini.