News
Kongamano la Kukuza Uelewa kuhusu masuala ya Ualbino lafanyika Kigoma
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Thobias Andengenye, amefungua kongamano la kuongeza uelewa kuhusu masuala ya Ualbino ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya kuelekea Siku ya Kimataifa ya Watu wenye Ualbino yanafanyika mkoani Kigoma.
Aidha, Akizungumza katika hotuba yake Juni 12, 2025, Mhe. Andengenye amesisitiza umuhimu wa taasisi zote za Serikali, Halmashauri, na wadau wa maendeleo kuhakikisha haki za msingi kwa watu wenye Ualbino zinazingatiwa ikiwa ni pamoja na elimu bora, huduma za afya, fursa za ajira, ulinzi na uwezeshaji wa kiuchumi na kijamii kwa kundi hilo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kitengo cha Watu wenye Ulemavu, Rasheed Maftah, amesema kuwa Ofisi ya Waziri itaendelea kushirikiana na wadau ili kuendelea kuimarisha huduma kwa watu wenye Ualbino.
Naye Rais wa Chama cha Watu Wenye Ualbino (TAS), Godson Mollel ameishukuru serikali kwa namna ambavyo imekuwa ikihudumia Watu wenye Ulemavu pia ameweka wazi mkakati wa chama hicho wa kutumia maadhimisho hayo kama jukwaa la kuelimisha jamii kuhusu masuala ya ualbino na kupunguza changamoto wanazokumbana nazo.
Itakumbukwa kuwa tarehe 13 Juni kila mwaka huadhimishwa Siku ya Kimataifa ya Uelewa kuhusu Ualbino, ikiwa ni siku maalum ya kuelimisha jamii kuhusu changamoto wanazokumbana nazo watu wenye Ualbino pamoja na kusherehekea mafanikio yao.
Maadhimisho huwa yanalenga kuimarisha juhudi za kutokomeza unyanyapaa na ubaguzi, kuhimiza usawa na ujumuisho wa watu wenye Ualbino katika nyanja zote za kijamii na kiuchumi.