Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Kanzidata na Mfumo wa Taarifa za Watu wenye Ulemavu zazinduliwa


✅ Ataka wenye ulemavu kutofichwa, washirikishwe katika maendeleo ya Taifa

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa, amewataka wazazi na walezi wasiwafiche watoto wenye ulemavu na wahakikishe wanafahamika mahali walipo, hali zao za ulemavu ili waweze kupata huduma stahiki na washiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa.

Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo leo (Jumamosi, Januari 25, 2025), wakati akizindua Kanzidata na Mfumo wa Taarifa za Watu Wenye Ulemavu unaotokana na matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya 2022, jijini Dodoma.

Waziri Mkuu amezitaka taasisi zote zinazotoa huduma kwa watu wenye ulemavu watumie takwimu hizo katika kutayarisha programu za kuwawezesha na kuwajengea uwezo watu wenye ulemavu kutumia fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali na wadau wa maendeleo kujiendeleza kiuchumi, kijamii na mazingira.

Aidha, amesema serikali imeweka mipango madhubuti ya kuwatengenezea mazingira rafiki watu wenye ulemavu nchini. Baadhi ya mipango hiyo amesema ni kutunga na kutekeleza sera, sheria na programu mbalimbali za kulinda haki, fursa, na maendeleo ya watu wenye ulemavu.

Katika kuendelea kuboresha sera ya Taifa na maendeleo ya huduma kwa watu wenye ulemavu ya 2004 na sheria ya watu wenye ulemavu namba 9 ya mwaka 2001, ambayo inamtaka kila mwajiri anatakiwa kuhakikisha asilimia tatu ya wafanyakazi wake wanakuwa watu wenye ulemavu.

Vile vile, kuwashirikisha watu wenye ulemavu na jamii yote kiujumla na sio kuwatenga. Hii ni pamoja na kuwajumuisha katika shule za wale wasio na ulemavu na sio kuwatenga katika shule zao peke yao. Kutengeneza mazingira rafiki kwa watu wenye ulemavu, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa majengo yanayoruhusu upatikanaji wa huduma rahisi kwa watu wenye ulemavu na kuwa na visaidizi vinavyowasaidia kuendesha maisha yao.

Pia, kuboresha huduma za afya, usawa wa kuhamasisha ajira na ushiriki wa watu wenye ulemavu katika masuala ya kiuchumi. Amesema serikali inafanya jambo hili kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Mfuko wa Kimataifa wa Watoto (UNICEF) na Umoja wa Mataifa (UN) na kuhakikisha watoto wote wenye ulemavu wanapewa kipaumbele kupata elimu katika ngazi zote kuanzia elimu ya msingi, sekondari, vyuo vikuu na elimu ya ufundi na mafunzo stadi.

Kwa upande mwengine, serikali imeendelea kuridhia na kutekeleza mikataba yote, maazimio yote na dira zote za kimataifa ambazo zinawagusa watu wenye ulemavu kama sehemu ya haki yao na kwamba utekelezaji unafanywa na serikali zote mbili, ya Jamhuri ya Muungano na ya Zanzibar.