Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

KANUNI ZA UTOAJI NA USIMAMIZI WA MIKOPO KWA VIJANA KUFANYIWA MABORESHO ZAIDI


Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Anthony Mavunde (wa tano kutoka kulia) akikabidhi mfano wa hundi ya Mkopo wa Shilingi Milioni 92 kwa ajili ya kuwezesha vikundi vya Vijana Wilayani Chato.

Serikali kufanyia maboresho kanuni za utoaji na usimamizi wa mikopo zitakazomwezesha kijana mmoja mmoja kupata fursa ya mkopo utakaowasaidia kuazisha ama kuendeleza miradi mbalimbali itakayowakwamua kiuchumi.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Anthony Mavunde wakati wa hafla ya kukabidhi hundi ya Shilingi Milioni 92 iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana.


Mheshimiwa Mavunde alieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuwawezesha vijana kiuchumi ili waweze kuanzisha au kuendeleza shughuli za uzalishajimali, hivyo ilianzisha kanuni za utoaji na usimamizi wa mikopo kwa vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu kwa lengo la kutoa mikopo yenye riba nafuu.


“Serikali kwa kuzingatia matatizo yanayowakabili vijana wake iliona vema kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ambao madhumini yake makubwa ni kuwapatia vijana mikopo yenye masharti nafuu itakayowasaidia kuanzisha au kuimarisha miradi yao,” alisema Mavunde

Aliongeza kuwa, kwa kulitambua hilo Serikali imeamua kuangalia utaratibu mzuri utakaokuwa unatoa fursa ya kuwezesha vijana kupata mikopo hiyo, ikiwemo suala la kumwezesha kijana mmoja mmoja kuwa na nafasi ya kupata mikopo hiyo.


“Mfano kijana akiwa ana mradi wake na akawa na vigezo vya kukopesheka ni vyema akapatiwa mkopo ili aweze kujiendeleza kiuchumi kwa kuwa atakuwa na uwezo wa kuzalisha ajira kwa vijana wengine,” alisema Mavunde

Alieleza kuwa hapo awali lengo la kutoa mkopo huo kwa vikundi vya vijana ilikuwa ni kuwezesha vijana kuendeleza miradi mbalimbali ya uzalishaji mali wanayoifanya pamoja na kuinua kipato chao na hatimae waweze kujikwamua kiuchumi.


Aliongeza kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu katika kulisimamia hilo imekuwa ikiendeleza ukuaji wa ujuzi wa vijana hao kwa kuanzisha Mpango wa kutoa mafunzo ya ujasiriamali na usimamizi wa biashara ili kabla ya kupatiwa mikopo waweze kuwa na ujuzi utakaowasaidia kuimarisha na kusimamia biashara zao kwa weledi na kuwa na mbinu za kukuza biashara zao.

Aidha, Naibu Waziri Mavunde amewataka vijana kuendelea kufanya kazi kwa kujituma na kutumia maarifa waliyonayo kubuni miradi mbalimbali ya uzalishaji mali ili waweze kukua kiuchumi.


“Nipongeze vikundi vya vijana vipatatavyo 12 kutoka wilaya ya Chato, Geita na Bukombe vilivyopatiwa Mkopo, hatua mliyofikia itachangia kwa kiasi kikubwa uanzishwaji wa viwanda vidogo vidogo vya ambavyo vitasaidia kutengeneza ajira na kuongeza ukuaji wa uchumi,” alieleza Mavunde

Kwa upande wake Mbunge wa Chato ambaye pia ni Waziri wa Nishati, Mhe. Medard Kalemani ameeleza kuwa jumla ya vikundi 783 vimeweza kusajiliwa katika mkoa wa Geita na baadhi ya vikundi hivyo vipo vya vijana wa wilaya chato ambavyo vimenufaika na mkopo huo uliowasaidia vijana kuanzisha na kuendeleza shughuli za kiuchumi ikiwemo ufugaji, kilimo, uchimbaji wa madini, uvuvi na biashara.


“Tunaipongeza sana Serikali kwa kutoa fursa ya mitaji kwa vijana ili waweze kuendeleza miradi ya vikundi vyao ambavyo vitachochea ukuaji wa uchumi wa chato,” alisema Kalemani

Sambamba na hayo Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu alieleza kuwa katika mkakati wa programu ya kukuza ujuzi inayosimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu ni vyema ikiwawezesha vijana kupata stadi za kazi katika utoaji huduma katika mahoteli ili kuendeleza na kukuza sekta ya utalii.“Uwepo wa hifadhi ya Burigi Chato imekuwa ni kichocheo cha ukuaji wa sekta ya utalii katika kanda ya ziwa, itakuwa vizuri nguvukazi ya vijana ikapata ujuzi stahiki utakaowawezesha kujua taratibu za uendeshaji wa sekta hivyo ambayo imekuwa ni kivutio kwa wageni wa nje,” alisema Kanyasu

Naye Mmoja wa vijana walionufaika na mkopo huo Bw. Leonard Ngaza ameishukuru Serikali kwa kuwapatia mkopo huo ambao utawasaidia kundeleza shughuli walizokusudia ili waweze kurejesha kwa wakati.