Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

KAMATI YA BUNGE YA KATIBA NA SHERIA YARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI WA MFUKO WA MAENDELEO YA VIJANA


Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria imeridhishwa na utekelezaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Vijana “Youth Development Fund” unaoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu katika kuchochea maendeleo ya shughuli za kiuchumi za vijana.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria akiongoza kikao cha kamati hiyo kilicholenga upokeaji wa taarifa ya utekelezaji wa Mfuko wa Maendeleo ya vijana, kilichofanyika Oktoba 25, 2019 katika Ofisi za Bunge, Jijini Dodoma. (Kulia) ni Katibu wa Kamati hiyo Bw. Stanslaus Kagisa.

Hayo yameelezwa na Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo ya kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Mhe. Najma Giga (Mb) wakati kamati hiyo ilipokutana kwa lengo la kufuatilia utekelezaji wa mfuko wa maendeleo ya vijana katika ukumbi wa Katiba na Sheria Bungeni Jijini, Dodoma.

Akizungumza wakati wa kikao hicho alisema kuwa Mfuko wa Maendeleo ya Vijana umekuwa ni kielelezo tosha kwa serikali katika kuonyesha dhamira ya dhati ya kuwasaidia vijana sambamba na kuendeleza miradi yao ya kiuchumi.

“Tunapongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kusimamia vizuri mfuko wa Maendeleo ya vijana kwa kuwa umeendelea kuwa chachu kwa vijana kuanzisha makampuni na vikundi vya uzalishaji mali katika ngazi ya halmashauri za wilaya, miji na manispaa ambazo zimeibua fursa ya ajira kwa vijana,” alisema Mheshimiwa Giga

Aliongeza kuwa kupitia mfuko huo vijana waendelee kuhamasishwa zaidi kujishughulisha na kubuni miradi mbalimbali ya kiuchumi na aliwataka kuongeza ubunifu katika shughuli zao za uzalishaji mali.

Aidha alitoa wito kwa vijana waliopata mikopo hiyo kuitumia vizuri mikopo hiyo kwa kuwa inamanufaa ili waweze kunufaika nayo pia kuifanya miradi yao kuwa endelevu.

Akielezea kuhusu mfuko huo wa Maendeleo ya Vijana Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Kazi, vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama alieleza kuwa lengo la kuanzishwa mfuko maendeleo ya vijana na Serikali mwaka 2013 ilikuwa ilikuwa kuwawezesha vijana kupata mitaji yenye masharti nafuu.

“Katika kipindi cha miaka mine ya Serikali ya awamu ya tano yaani mwaka 2015 – 2018 jumla ya bilioni 2 zimetolewa katika vikundi vya vijana 533 vyenye idadi ya vijana 3,780 katika halmashauri 128 nchini,” alisema Mhagama

Akielezea miradi ya vijana iliyoweza kunufaika na mikopo ya mfuko huo ikiwemo Kilimo, Ufugaji, Viwanda vya kuchakata (Ngozi, Madini, kusindika mazao ya chakula, vifaa vya ujenzi, kutengeneza taulo za kike, kusindika chakula cha mifugo), Makampuni yanayotoa huduma za mawasiano, makampuni yanayotoa huduma za kifedha na makampuni yanayotoa huduma za elimu.

Alieleza kuwa Serikali inaendelea kuwahamasisha vijana pamoja na wenye ulemavu kuendelea kuchangamkia fursa ya mikopo hiyo ambayo imekuwa kielelezo katika kubadili mtazamo wa vijana kujijengea dhana ya kujitegemea na kukuza vipato vyao.

“Mwaka huu wa fedha 2019/2020 Serikali inatarajia kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 850 kwa vikundi vya vijana 224 katika halmashauri za wilaya 56, kwa dhamira hii njema ya serikali ni wakati muafaka vijana wakawa wabunifu katika kuanzisha miradi yenye tija itakayowawezesha kukopesheka,” alieleza Mhagama

Aidha aliwashauri vijana walionufaika na mfuko huo wahakikishe wanarejesha mikopo hiyo kwa wakati ili mfuko huo uweze kuwa endelevu na manufaa kwa vijana.