News
Waziri Ridhiwani: Serikali inaendelea kuzingatia maslahi ya Wafanyakazi
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Ridhiwani Kikwete amesema Serikali itaendelea kuzingatia maslahi ya wafanyakazi ikiwamo kuongeza kikokotoo ambacho kwa sasa kimefikia asilimia 40 na kinalipwa vizuri.
Mhe. Kikwete ameyasema hayo Januari 15, 2025 alipokuwa akifungua kikao cha Baraza Kuu la Chama Cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU) jijini Dodoma.
Amesema serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kushirikiana na chama hicho na kutatua changamoto zinazowakabili Watumishi wa Umma ikiwamo wa Serikali za Mitaa.
Aidha, amewataka Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kulipa madai ya watumishi ikiwamo fedha za likizo, uhamisho na posho ya madaraka kwa Maofisa Watendaji wa Kata.
Pamoja na hayo, ameahidi kukutana na Mawaziri wa kisekta ili kutafutia ufumbuzi wa hoja zilizotolewa na chama hicho ili kuleta ustawi mzuri wa wafanyakazi.
Naye, Mwenyekiti wa TALGWU Taifa ambaye pia ni Rais wa Shirikisho la Vyama Vya Wafanyakazi (TUCTA), Tumaini Nyamhokya amepongeza serikali kwa kuendelea kutatua kero zinazowakabili wafanyakazi walipo kwenye mamlaka hizo ikiwamo kilio cha muda mrefu cha watumishi waliokuwa wanalipwa mishahara kupitia mapato ya ndani ya halmashauri ambao kwasasa wanalipwa kupitia Mfuko Mkuu wa serikali.