Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Vijana Wasisitizwa Kuzingatia Maadili na Uzalendo


Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi amewataka vijana nchini kuwa wazalendo na kuzingatia maadili ili kuwa taifa bora sasa na baadae.

Mhe. Katambi ametoa rai hiyo wakati akifungua kongamano la vijana la kisayansi lililofanyika Mkoani Morogoro kwa lengo la kujadili na kupata elimu kuhusu mambo mbalimbali yanayohusu mapambano dhidi ya UKIMWI.

“Vijana wana mchango mkubwa katika ujenzi wa taifa na wanaweza kutoa mchango mkubwa zaidi iwapo watafanya shughuli zao kwa kuzingatia uzalendo, weledi na maadili,” amesema

Aidha, ameeleza kuwa Utafiti wa Viashiria vya UKIMWI mwaka 2016/2017 nchini, umeonyesha kuwa moja ya makundi yaliyo nyuma katika kufikia malengo ni vijana huku wengi wenye umri mdogo hawajui hali zao za maambukizi ukilinganisha na watu wenye umri mkubwa, hali inayosababidha vijana wenye virusi vya UKIMWI kutoanza dawa za ARV mapema.

Vile vile, Mhe. Katambi ametoa rai kwa vijana nchini kujitokeze kwa wingi katika huduma za upimaji wa VVU kwa hiari sambamba na kupiga vita mmomonyoko wa maadili.