Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Vijana wahimizwa kutumia majukwaa kutoa maoni ya dira ya Taifa ya Maendeleo 2050


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Ridhiwani Kikwete amewataka Vijana kutumia fursa ya Kongamano la Vijana linalolenga Uhakiki wa Rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, kutoa maoni yatakayojumuishwa kwenye Dira ya Taifa ya maendeleo 2050.

Mhe. Ridhiwani amebainisha hayo Desemba 18, 2024 wakati wa Kongamano hilo lililofanyika katika ukumbi wa mikutano uliopo Makumbusho ya Taifa, Posta Jijini Dar es Salaam.

Amesema Serikali imeendelea kuwekeza katika maeneo mengi ya elimu, afya, na mambo yote ya ustawi wa jamii ili kuhakikisha vijana wanafaidika fursa zinazotolewa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Nini maoni yenu vijana juu ya haya yanayofanyika leo kwa ajili ya kesho yetu, hili ndilo jambo tunalolitaka kulisikia kutoka kwenu vijana ili tuweze kuona kipi cha kufanya”, amesema.