Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Ubunifu wa Vijana Wapigiwa Chapuo


* Viongozi Wahumizwa kutambua Ubunifu wa Vijana.

SERIKALI imesema vijana ni nguzo muhimu katika ujenzi wa maendeleo ya taifa hivyo ni vyema viongozi wakatambua ubunifu wao ili kuwainua kiuchumi.

Amesema hayo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama ambaye alimwakilisha Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa wakati wa uzinduzi wa Wiki ya vijana Kitaifa iliyofanyika uwanja wa CCM Stendi ya Zamani, Babati Mkoani Manyara, tarehe 10 Oktoba, 2023.

Aidha, Waziri Mhagama amepongeza mwamko wa Vijana jinsi walivyojitokeza kuhudhuria katika Wiki yao inayowapa fursa ya kutambua mambo mbalimbali yanayofanywa na vijana wenzao nchini.

"Binafsi nimefurahishwa na muamko wa vijana jinsi mlivyojiyokeza na kuonyesha kazi zenu, nimepita katika mabanda mbali mbali nimejionea kazi zenu za mikono na kwakweli vijana ni nguvu kazi ya Taifa letu,"

Vilevile Mhe. Waziri Mhagama ametoa wito kwa benki mbalimbali nchini kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa vijana ili waweze kuanzisha shughuli za kiuchumi na kufikia ndoto zao.

Kwa Upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako amesema lengo la kuanzishwa kwa wiki hiyo ni kuhamasisha vijana na kuwakutanisha ili waweze kubadilishana mawazo juu ya namna ya kujiinua kiuchumi.

"Ni fursa kwa Serikali na Wadau kutambua mchango mzuri wa vijana kwa maendeleo ya nchi yetu," amesema

Akizungumza awali Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga amemshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt, Samia Suluhu Hassan kwa kuchagua Manyara kuwa Mwenyeji wa Kilele cha Madhimisho ya Siku ya vijana kitaifa, Mwenyeji wa Misa Maalumu ya Kumbukizi ya Baba wa Taifa na Killele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru.

Maadhimisho ya wiki ya vijana Kitaifa ya Mwaka 2023 yanayofanyika Mkoani Manyara, kauli mbiu yake ni,” Vijana na Ujuzi Rafiki kwa Mazingira na Maendeleo Endelevu”.