Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Timu ya Wakurugenzi Ofisi ya Waziri Mkuu yafanya ziara Mgodi wa Barrick - Bulyankulu


TIMU ya Wakurugenzi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu wamefanya ziara ya kikazi ya siku mbili katika mgodi wa Barrick-Bulyankulu kuangalia namna unavyotoa fursa za ajira, uwezeshaji vijana na ukuzaji tija.

Akizungumza leo baada ya kutembelea eneo la uzalishaji la mgodi huo (underground), Mwenyekiti wa msafara wa Wakurugenzi hao ambaye ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Ukuzaji Tija wa Ofisi hiyo, Yohana Madadi, amesema ziara hiyo inaangalia shughuli zinazofanywa, fursa za ajira na zilizotengenezwa kwa jamii kutokana na uwekezaji huo.

“Tumejifunza mambo mengi tumeona kuna usalama mahali pa kazi ndani ya mgodi, tumeona fursa za ajira, maeneo yanayohitaji ujuz, sisi kama wadau wa kusimamia eneo la kazi tutakaporudi tutaendelea kushirikiana ili uwekezaji huu uendelee kuwa na tija kwa watanzania,”amesema.

Naye, Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Ajira, Joseph Nganga, ameshauri mgodi kuendelea kuwachukua wahitimu wa kujitolewa wa fani zinazohitajika kwenye mgodi huo ili kupata uzoefu utakaowajengea uwezo wa kupata ajira kwenye maeneo mengine.

Kwa upande wake, mmoja wa wasimamizi wa mgodi huo katika uzalishaji, Andi Mwakibete, ameshukuru Wakurugenzi kwa kutembelea mgodi huo na wameendelea kusimamia usalama mahali pa kazi kwa kuweka mitambo ya kisasa na kuondokana na mashine za kizamani ambazo hazikuwa salama kwa wafanyakazi.

Timu hiyo Desemba 2, 2023 itahitimisha ziara yake katika mgodi wa Barrick- Buzwagi mkoani Shinyanga.