Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Serikali kuendelea kuunga mkono Wenye Ulemavu


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Ridhiwani Kikwete amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwaunga mkono Watu wenye Ulemavu kwa kusimamia na kulinda maslahi ya kundi hilo.

Amesema hayo leo (Jumanne, Desemba 17, 2024) wakati akifungua kikao cha Baraza la Ushauri la Taifa kwa Watu wenye Ulemavu kilichofanyika katika ukumbi wa PSSSF, Jijini Dodoma.

Mhe. Ridhiwani amesema kuwa, Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan anatambua na kuthamini mchango wa Watu wenye Ulemavu katika kukuza maendeleo ya Taifa.

"Maelekezo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha wananchi wote wanashiriki katika ujenzi wa taifa, ambapo Watu wenye Ulemavu wanashiriki pia katika ujenzi wa taifa lao," amesema

Vile vile, Mhe. Waziri Ridhiwani Kikwete amesema kuwa serikali kupitia wizara yenye dhamana ya kushughulikia masuala ya Watu wenye Ulemavu ilizindua Mpango kazi wa Taifa wa haki na ustawi wa Watu wenye Ualbino na Mkakati wa Taifa wa Teknolojia saidizi hivyo, amewataka wajumbe wa baraza hilo katika uandaaji wa sera ya taifa ya maendeleo na huduma kwa watu wenue Ulemavu kuzingatia mambo yote muhimu ya kundi hilo kama ilivyo katika mpango na mkakati huo.

Aidha, kikao kazi hicho kililenga kupitia rasimu ya Sera ya Taifa ya Maendeleo na Huduma kwa Watu wenye Ulemavu ya Mwaka 2024.