Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Serikali kuendelea kuthamini haki na ustawi wa Watu Wenye Ulemavu


SERIKALI inaendelea kuyapa kipaumbele masuala ya Watu wenye Ulemavu, kuthamini haki na ustawi wao kwa kutekeleza shughuli mbalimbali ikiwemo, kufanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Maendeleo na Huduma kwa Watu wenye Ulemavu ya mwaka 2004.

Amesema hayo leo Disemba 1, 2023 jijini Dodoma, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi, wakati akizindua Kongamano la Watu Wenye Ulemavu lilolenga kujadili masuala mbalimbali kuhusu wenye Ulemavu, kuelekea Kilele cha siku ya Kimataifa ya Watu wenye Ulemavu.

Vile vile, amesema serikali imeendelea kukamilisha Mwongozo wa Ufikivu wa miundombinu, pia Mwongozo wa uanzishwaji, uendeshaji na usimamizi wa vyuo vya ufundi stadi na marekebisho kwa Watu wenye Ulemavu.

Sambamba na hayo, Mhe. Katambi amesema elimu imeendelea kutolewa kwa jamii kuhusu ujumuishwaji wa masuala ya Watu wenye Ulemavu.

Kwa upande mwengine, Naibu Waziri Katambi amepongeza Watu wenye Ulemavu kwa kumuunga Mkono Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuwaletea wananchi maendeleo.

Naye, Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma kwa Watu wenye Ulemavu Bw. Rasheed Maftah, amesema kuwa zoezi la mapitio ya sera ya Maendeleo ya watu Wenye Ulemavu limeanza.