Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Serikali itaendelea kutekeleza programu za kuwawezesha vijana - Katambi


Serikali imesema itaendelea kutekeleza programu za kuwawezesha vijana ikiwemo Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi ambayo inalenga kuimarisha ujuzi wa vijana ili waweze kushindana kikamilifu katika soko la ajira.

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi leo Disemba 6, 2023 Mkoani Morogoro wakati wa kikao kazi cha kupokea taarifa za utafiti wa soko la ajira kwa vijana kupitia mradi wa USAID Kijana Nahodha.

Katambi amesema Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameweka mazingira wezeshi ya kisera ili kuhakikisha vijana wanashiriki katika shughuli za kiuchumi ikiwemo Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya Mwaka 2007, Sera ya Taifa ya Ajira ya Mwaka 2008 na Sera ya Kilimo kupitia Mkakati wa kuwahusisha vijana katika Kilimo ambazo tayari zimewezesha kuanzisha programu za uwezeshaji kwa Vijana.

“Tafiti hizi zinatuwezesha kuelewa hali ya soko la ajira kwa ujumla na mahitaji ya waajiri kama vile, ujuzi wanaohitaji na namna wanavyoajiri. Hivyo, Tafiti hizi zina mchango mkubwa katika kubuni na kutekeleza programu za kuwawezesha vijana. Pia tafiti hizi zinatusaidia kuwaelewa vijana wa Kitanzania, namna walivyogawanyika, mahitaji na matarajio yao” amesema Katambi.

Awali akitoa salamu Mkurugenzi wa Mradi wa USAID Kijana nahodha Neemiah Kahakwa amesema kupitia mradi huo vijana wanapatiwa elimu ya ujasiriamali, ufundi, biashara, stadi za maisha na mbinu za utafutaji na ukuzaji ujuzi.

Pia, amesema mradi huo umejikita katika kuimarisha Afya ya mwili na akili kwa vijana ambapo kwa mwaka 2023/2024 jumla ya vijana 4,423 wamefikiwa katika Mkoa wa Morogoro, Dar es salaam na Zanzibar.