News
Serikali inachukua hatua mahsusi kuendeleza biashara changa, bunifu kwa Vijana
Serikali inaendelea kuchukua hatua mahususi kuhakikisha mazingira ya biashara changa na bunifu (Startups) kwa vijana kwa kuwa na sera itakayotoa mwongozo wa kukuza, kuendeleza na kuimarisha mifuko ya kusaidia vijana.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Ridhiwani Kikwete wakati wa hafla ya kufunga Wiki ya Makampuni bunifu leo Desemba 20, 2024 Jijini Dar es salaam.
Aidha, Mhe. Ridhiwani amesema Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua umuhimu wa Startups katika kutengeneza mazingira bora ya kukuza makampuni bunifu ya vijana, hivyo itaendelea kutoa mitaji ya awali ya kukuza miradi yao.
Vile vile, amesema serikali imeendelea kushirikiana na wabia wa maendeleo kwa lengo la kuhakikisha vijana wabunifu wanaendelezwa na tayari imefanya mazungumzo na Benki ya maendeleo ya Afrika kwa lengo la kuanzisha Taasisi itakayowawezesha Vijana wabunifu na wajasiliamari kuendeleza shughuli zao za ubunifu.