Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

​Ridhiwani: Kima cha Chini Mshahara Sekta Binafsi Chaongezeka


Serikali ya Awamu ya Sita imefanikiwa kutangaza nyongeza ya Kima cha chini cha Mshahara kwa sekta binafsi ambapo kimepanda kwa asilimia 33.4 hatua inayolenga kuongeza tija na kukuza ari ya wafanyakazi kwa kuongeza tija na uzalishaji.

Akitangaza Amri hiyo, leo (17 Oktoba 2025) Jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa Habari, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu -Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Ridhiwan Kikwete amesema mchakato wa upangaji wa Kima kipya cha chini cha mshahara umekamilika na kwamba umezingatia mamlaka aliyopewa chini ya Kifungu cha 39 (1) cha Sheria ya Taasisi za Kazi, Sura 300.

“Kwa mujibu wa Amri hiyo, Sekta za Kima cha chini cha Mshahara zimeongezeka kutoka 13 za mwaka 2022 hadi 16 kwa mwaka 2025 na kutoka sekta ndogo 25 za mwaka 2022 hadi 46 kwa mwaka 2025.

Aidha, Kima cha chini cha mshahara kimeongezeka kwa wastani wa asilimia 33.4 kutoka Shilingi 275,060/= hadi 358,322/= na kitaanza kutumika rasmi tarehe 1 January, 2026”, amesema Waziri Ridhiwani Kikwete.

Kwa mujibu wa Waziri Ridhiwani , Amri ya Kima cha Chini cha Mshahara imegusa sekta za kilimo, afya, mawasiliano, usafirishaji, hoteli, madini, biashara na viwanda, shule binafsi, huduma za ulinzi binafsi, nishati, uvuvi na huduma ya baharini, michezo na utamaduni pamoja na huduma nyinginezo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Kima cha Chini cha Mshahara kwa Sekta Binafsi Dkt. Suleiman Rashid Mohamed amesema mchakato wa majadiliano ulikuwa shirikishi ambapo vyama vya wafanyakazi, waajili na waajiliwa vilishiriki kikamilifu katika hatua zote.

Naye Naibu Katibu Mkuu Shirikishio la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) Rehema Ludanga amesema kitendo cha Serikali kutangaza Amri ya kupanda kwa mishahara kwa kima cha chini cha sekta binafsi ni faraja kwa wafanyakazi nchini kwani kimeonesha dhahili namna Serikali inavyothamini maslahi ya wafanyakazi nchini.

Rehema aliongeza kusema ni wakati sasa waajili wote katika sekta binafsi kutekeleza amri hiyo kwa kupandisha mishahara ikibidi zaidi ya kiwango kilichotangazwa ili kuongeza maslahi bora ya wafanyakazi wao .

Suzanne Ndomba-Doran Afisa Mtendaji Mkuu Chama cha Waajili Tanzania (ATE) ameeleza kuwa Chama hicho kilishiriki kikamilifu kwenye mchakato kupitia kamati ya wataalam ambapo maoni yote yaliyokusanywa toka mikoa yote nchini na yamefanyiwa kazi hatua inayotoa urahisi wa utekelezaji wa amri hiyo.

Aidha, Mtendaji Mkuu huyo amewasihi waajiri kutumia muda huu kabla ya kufika tarehe 01 Januari 2026 kufanya mazungumzo yatakayopelekea kubadilisha ulipaji wa mishahara kwa mujibu wa amri iliyotangazwa na Serikali na kwamba ATE itaendelea kutoa elimu na taarifa kwa waajiri wote nchini kutekeleza amri hiyo.