Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Profesa Ndalichako Ataka Mawakala Binafsi wa Huduma za Ajira Kuzingatia Matakwa ya Sheria za Kazi


Waziri wa Nchi - Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako amewataka Mawakala binafsi wa huduma za ajira kuzingatia matakwa ya kisheria kwa kusajili makampuni yao na kutekeleza majukumu kwa kuzingatia wigo wa kisheria.

Prof. Ndalichako ametoa agizo hilo Oktoba 23, 2023 Jijini Dar es salaam katika Mkutano wa Mawakala binafsi wa Huduma za Ajira, ulio lenga Kuongeza ufanisi wa shughuli za mawakala binafsi wa ajira na kuweka mikakati ya kuongeza fursa za ajira kwa watanzania nje ya nchi.

Amesema Serikali imeruhusu Mawakala Binafsi kuunganisha watanzania na fursa za ajira nje ya nchi ambapo kwa mwaka wa fedha 2022/23 takribani Mawakala 83 walisajiliwa, 56 kati yao wamehuisha leseni zao kwa mwaka 2023/24.

Aidha, amewapongeza Mawakala walio waunganisha watanzania na fursa za ajira nje ya nchi na kuwezesha ajira za staha 1,243 ambazo kwa miezi 12 zimewapatia watanzania takribani Shilingi billioni 16.

Amesema Serikali itaendelea kuimarisha usimaizi na udhibiti wa shughuli za Wakala wa Huduma za Ajira ili kutekeleza shughuli zao kwa weledi na uadilifu hivyo kuchangia katika kupunguza tatizo la ajira nchini, kukuza uchumi na kuchangia pato la Taifa.

Akizungumza katika Mkutano huo, Katibu Mkuu Ofisi hiyo Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema ataweka miundombinu nzuri ya kuwapeleka watanzania nje ya nchi na kutatua changamoto wanazokumbana nazo mawakala.