Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Prof. Ndalichako Azitaka Taasisi za Umma kuwa na Wataalamu wa Lugha ya Alama


WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako amezitaka Taasisi za Umma kuhakikisha zinakuwa na wataalam wa lugha ya alama ili inapohitajika kutoa huduma kwa wateja wenye Uziwi pasiwe na kikwazo katika kuwasiliana.

Wito huo umetolewa na Waziri Ndalichako jijini Dodoma, leo Septemba 20, 2023 wakati akizungumza na waandishi wa Habari Jijini Dodoma kuhusu maandalizi ya Maadhimisho ya Wiki ya Viziwi yanatarajia kufanyika tarehe 25 hadi 30 Septemba, 2023 Mkoani Mbeya.

Akitaja lengo la kuanzishwa kwa wiki ya Viziwi Duniani ni kutoa fursa Watu wa Jamii ya Viziwi kushiriki kwenye shughuli mbalimbali za Maendeleo kwa kushirikiana na jamii zinazowazunguka bila kuwepo vikwazo vyovyote ikiwemo vikwazo vya mawasiliano yao.

Aidha, Profesa Ndalichako amesema Serikali inayoongowa na Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kwa ajili ya ustawi wa Watu wenye Ulemavu nchini ikiwa ni pamoja na Watu wa Jamii ya Viziwi ambapo elimu imeendelea kutolewa kwa umma na wadau mbalimbali kuhusu changamoto zinazo kabili kundi hilo ikiwemo kuhamasisha utamaduni wa kuwasiliana kwa kutumia lugha ya alama.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Viziwi Tanzania (CHAVITA), Adam Shaibu ameishukuru serikali kwa kutoa ushirikiano na kuwamini Watu wenye Ulemavu ikiwemo kuwapatia fursa za kiuchumi, kijamii, kiuongozi na ajira.

Kauli mbiu ya maadhimisho hayo mwaka huu 2023 ni “Dunia ambayo Popote Walipo Viziwi Wanaweza Kutumia Lugha ya Alama.”

Kauli mbiu hii inalenga kila taasisi inayotoa huduma kwa jamii inakuwa na mkalimani wa lugha ya alama sambamba na kuwajengea uwezo watumishi wake kuwa na uelewa wa lugha ya Alama.