Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Prof. Ndalichako aitaka TaESA kuibua fursa za Ajira kwa Watanzania


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako amekiagiza Kitengo cha Huduma za Ajira cha ofisi hiyo (TaESA) kuibua fursa za ajira kwa watanzania na kusimamia vibali vya mawakala binafsi wanaopeleka vijana nje ya nchi kwenye kazi zenye staha.

Mhe. Ndalichako akizungumza Septemba 14, 2023 na watumishi wa kitengo hicho jijini Dar es salaam, Waziri Ndalichako amewataka TaESA kufanya mazungumzo na nchi rafiki kupitia Balozi za Tanzania ili kupata fursa za ajira.

Aidha, amesisitiza TaESA kuboresha tovuti yao kwa kuonyesha fursa za ajira kwa vijana wa kitanzania ikiwamo zinazotangazwa na sekta binafsi na taasisi zingine.

Naye, Mkurugenzi wa Kitengo hicho, Joseph Nganga, amesema TaESA inatoa huduma za ushauri katika soko la ajira za ndani na nje ya nchi, kutambua mahitaji ya waajiri na kuwaunganisha watafuta kazi na waajiri ili wapate uzoefu wa kazi.

Amesema kwa mwaka wa fedha 2023/24 serikali imetoa Sh.bilioni 2.5 kwa TaESA ili kuwezesha shughuli mbalimbali ikiwamo mafunzo ya kushindania fursa za ajira.