Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Nchi Wanachama EAC kuthamini mchango wa sekta isiyo rasmi


Serikali za Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zitaendelea kuthamini mchango unaotolewa na sekta isiyo rasmi katika kuleta maendeleo ya nchi hizo ikiwemo kukuza ajira.

Kauli hiyo imetolewa na Mwakilishi wa Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Brigedia Jenerali Salum Mnumbe wakati akizungumza kwenye Maadhimisho ya Siku ya Tanzania maarufu kama Tanzania Day yaliyofanyika leo tarehe 10 Desemba 2023 jijini Bujumbura, Burundi ikiwa ni sehemu ya shughuli za Maonesho ya 23 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki yanayoendelea jijini hapa.

Amesema kuwa, Nchi Wanachama wa Afrika Mashariki zilianzisha maonesho hayo kwa kutambua na kuthamini mchango unaotolewa na sekta isiyo rasmi katika kukuza maendeleo ya nchi hizo ikiwemo kuzalisha fursa za ajira kwa wingi na kuzalisha bidhaa zinazotumiwa zaidi na wananchi.

Vile vile, amewataka kuongeza bidii katika kuzalisha bidhaa bora kwa viwango vya kimataifa na kuzitangaza bidhaa hizo ndani na nje ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kuongeza wigo wa soko.

Kwa upande mwengine, ametumia fursa hiyo kuwapongeza na kuwashukuru wajasiriamali kutoka Tanzania kwa kuandaa bidhaa zenye ubunifu, ubora wa hali ya juu na zenye asili ya kitanzania.

Siku ya TANZANIA DAY iliambatana na shughuli mbalimbali ikiwemo wajasiriamali wa Tanzania kuonesha utamaduni wa Tanzania pamoja na bidhaa mbalimbali zinazozalishwa nchini. Miongoni mwa shughuli hizo ni pamoja na maonesho ya mavazi ya asili, ngoma za asili na burudani.

Maonesho ya 23 yamewashirikisha wajasiriamali 1,500 kutoka nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, wakiwemo 259 kutoka Tanzania yanafanyika kwa mara ya tatu nchini Burundi tangu kuanzishwa kwake mwaka 1999.