Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Naibu Waziri Katambi aeleza hatua za Uanzishwaji Mfuko wa Taifa wa Watu wenye Ulemavu


Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi, amesema serikali imechukua hatua mbalimbali katika uanzishwaji wa Mfuko wa Taifa wa Watu wenye Ulemavu kwa kuandaa mwongozo wa usimamizi, uratibu na uendeshaji na kufungua akaunti ya mfuko husika.

Hata hivyo, mfuko huo bado haujaanza kutoa huduma kutokana na maelekezo ya kuunganisha mifuko yote ya uwezeshaji wananchi kiuchumi yaliyotolewa mwaka 2020.

Mhe. Katambi ametoa kauli hiyo bungeni leo Aprili 27, 2023 alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Mhe. Stella Ikupa ambaye amehoji lini mfuko huo utaanza kufanya kazi.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Katambi amesema mfuko huo umeanzishwa kwa mujibu wa kifungu cha 57 cha Sheria ya Watu Wenye Ulemavu namba 9 ya Mwaka 2010.

"Katika kutimiza adhima ya Serikali ya uanzishwaji wa mfuko huu, hatua mbalimbali zimeshachukuliwa na Serikali ikiwemo uandaaji wa mwongozo wa usimamizi, uratibu na uendeshaji wa mfuko husika pamoja na kufunguliwa kwa akaunti ya mfuko," amesema.

Amesema pamoja na kukamilika kwa hatua zote muhimu za mfuko kuanza kutekeleza majukumu yake bado haujaanza kutokana na maelekezo ya kuunganisha mifuko yote ya uwezeshaji wananchi kiuchumi yaliyotolewa mwaka 2020.

"Zoezi hili liliambatana na tathmini ya ufanisi wa utendaji wa mifuko. Aidha, tathimini hii punde itakapokamilika, wadau wote wataarifiwa juu ya uanzishwaji na uendeshwaji wa mifuko hiyo ukiwamo Mfuko wa Taifa kwa Watu wenye Ulemavu," amesema Mhe. Katambi.