Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Mhe. Katambi awahamasisha Vijana na Wanawake kuchangamkia fursa za Kiuchumi


Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi amewataka vijana wa kike na wanawake nchini kuchangamkia fursa zilizopo ili kujikwamua kiuchumi.

Mhe. Katambi ameyasema hayo wakati alipomwakilisha Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa katika ufunguzi wa Mkutano wa 11 wa Maafisa Watendaji Wakuu Wanawake Tanzania uliofanyika jijini Dar es Salaam.

“Wanawake ni jeshi kubwa na Serikali ina matarajio makubwa na kundi hilo katika kuweza kushiriki vema kukuza na kuimarisha uchumi wa nchi yetu na jamii kwa ujumla,” amesema.

Aidha, ameeleza kuwa Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inatambua kuwa rasilimali watu ni nyenzo muhimu ya kuleta maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii.

Halikadhalika, Naibu Waziri Katambi amewasilisha maagizo ya Waziri Mkuu kwa Bodi ya Wakurugenzi ya Tanzania Women CEOs Roundtable ambapo ameitaka TWCR kushirikiana na Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) ili kubaini maeneo yenye uhitaji na kuandaa programu za kujenga uwezo, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake, Watoto na Makundi Maalum iimarishe kanzidata ya Viongozi na Maafisa Watendaji Wakuu Wanawake katika Sekta ya Umma pamoja na Sekta Binafsi.

Vilevile, Bodi hiyo na Taasisi za Sekta Binafsi ziangalie namna ya kujenga uwezo kwa wataalam wabobezi wanawake katika uendeshaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ya Kitaifa, kutengeneza mikakati itakayoleta matokeo chanya katika ustawi wa wanawake na Taifa kwa ujumla, imarisheni huduma za uwezeshaji katika kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na makundi ili kupunguza umaskini na Utoaji na tuzo na vyeti kwa Maafisa Watendaji Wakuu Wanawake wanaofanya vizuri kwenye Taasisi na sekta mbalimbali ni jambo la msingi katika kuhamasisha ushiriki wa wanawake wengi kwenye shughuli za kuchumi nchini.

Kwa upande wake, Mwanzilishi na Mtendaji Mkuu wa Jukwaa la Maafisa Watendaji Wakuu Wanawake Tanzania (TWCR), Bi. Emma Kawawa ametoa wito kwa wanawake kuwa wajasiri, kujiamini na kuthubutu katika kuanzisha Biashara ili kujikomboa kiuchumi.