Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Katibu Mkuu Luhemeja atoa siku 100 PSSSF kukamilisha awamu ya pili ujenzi kiwanda cha bidhaa za ngozi


Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhandisi Cyprian Luhemeja ametoa siku 100 kwa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Wafanyakazi wa Umma (PSSSF) kuhakikisha Awamu ya Pili ujenzi wa kiwanda cha kuchakata Bidhaa za Ngozi Kilimanjaro unakamilika na kuanza kufanya kazi ifikapo Julai 2024.

Agizo hilo amelitoa leo Februari 22, 2024 alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi katika kiwanda hicho cha Kilimanjaro International Leather Industries Ltd (KLICL) ikiwa ni sehemu ya kukagua maendeleo ya miradi inayotekelezwa na serikali kupitia Ofisi hiyo.

Mhandisi Luhemeja amesema kukamilika kwa kiwanda hicho kutaongeza thamani ya zao la ngozi ghafi, kufungua fursa za soko la uhakika la Ngozi kutoka kwa wafugaji, kuongeza ajira kwa vijana na mapato ya fedha za ndani na za kigeni.

Kwa upande mwengine, amesema kuwa ameridhishwa na ubora wa bidhaa zinazozalishwa kiwandani hapo na kutoa wito kwa watanzania kuwa na tamaduni za kuthamini bidhaa zinazo zalishwa nchini.

Akizungumza awali, Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Abdul-Razaq Badru amesema amepokea maagizo hayo na kuahidi kuwa PSSSF kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza watahakikisha wanakamilisha awamu ya pili ya ujenzi wa kiwanda hicho ili watanzania wanufaike na mradi huo.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda hicho Mhandisi Saiba Edward amesema mradi huo pamoja na mambo mengine, utaongeza kipato kwa wakazi wa Kilimanjaro na Mikoa jirani kupitia fursa za uzabuni, uwakala na usambazaji wa bidhaa.

Kwa upande wake Kamishina Msaidizi wa Jeshi la Magereza Frank Mwakijungu amebainisha kuwa Magereza ni mbia wa utekelezaji wa Mradi huo hivyo watasimamia ujenzi wa kiwanda hicho ili kikamilike kwa wakati kwa manufaa ya watanzania.