Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Kamati ya Bunge Yapongeza Serikali kwa Utekelezaji wa Mradi wa Mzizima Tower


KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imeipongeza serikali kwa kuuendeleza Mradi wa jengo la Kitega Uchumi ‘Mzizima Tower’ unaomilikiwa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Fatuma Toufiq ameyasema hayo Novemba 14, 2023 jijini Dar es salaam katika ziara ya kamati hiyo ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo ambao umefikia asilimia 89.

Amesema mradi huo ulisimama kwa muda mrefu na kwamba maelekezo na busara za Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan zimefanikisha kuendelea kutekelezwa mradi huo.

“Tunaishukuru serikali chini ya Rais Samia kwa kuona kwamba uwekezaji huu uendelee kuwepo ili tija kwa watanzania ipatikane ikiwamo upatikanaji wa ajira na kukuza pato la taifa,”amesema.

Naye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Joyce Ndalichako, amemshukuru Rais Samia kwa dhamira yake ya kukuza uwekezaji nchini na kwamba mradi huo ulianza tangu Mwaka 2013 na ulisimama lakini baada ya Rais Samia kuingia madarakani alielekeza miradi yote ifanyiwe tathmini na ikamilishwe.

“Kukamilika kwa mradi huu kutafungua fursa za ajira, tunategemea hapa zaidi ya wafanyakazi 300 ambao watakuwa na ajira za moja kwa moja na zingine zisizo za moja kwa moja zitapatikana, pia mradi huu utakuza fursa za utalii wa mikutano,”amesema.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi, amesema maoni yote yaliyotolewa na wajumbe wa kamati serikali itaendelea kuyafanyia kazi ili kuleta ufanisi kwenye mradi huo.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba, amesema mradi huo ulianza mwaka 2013 kwa gharama ya sh.bilioni 232.34 na utakapokamilika unatarajia kulipa ndani ya kipindi cha miaka 15.