News
Waziri Kikwete awataka Waajiri kutumia Teknolojia na Mifumo bora kwa Usalama na Afya Mahali pa Kazi
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Ridhiwani Kikwete amewataka waajiri nchini kutumia teknolojia za kidijitali na mifumo bora katika shughuli za uzalishaji inayozingatia kulinda afya na usalama wa wafanyakazi wakiwa kazini na kuongeza tija katika uzalishaji.
Aidha, amesema mchango wa teknolojia mpya mbalimbali kama Roboti za kisasa na Akili Mnemba (AI) zinazotumika katika uzalishaji na utoaji huduma huleta mapinduzi na uboreshaji wa usalama na afya kazini, hivyo amewataka wafanyakazi na waajiri kujiandaa na kuzoea teknolojia hizo ili kuongeza ufanisi.
Mhe. Ridhiwani Kikwete amesema hayo leo Aprili 28, 2025 katika hafla za kilele cha maadhimisho ya siku ya kimataifa ya usalama na afya mahali pa kazi iliyofanyika katika viwanja vya Mandewa, Mkoani Singida.
Amesema, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa mstari mbele katika kuhakikisha kuwa nguvu kazi ya taifa inalindwa kwa kuendelea kuimarisha taasisi ya OSHA ikiwemo kuongeza idadi ya watumishi na kuongeza vifaa vya ukaguzi na uchunguzi wa afya za wafanyakazi. Lengo ni kuhakikisha kuwa wafanyakazi wanapata huduma za usalama na afya mahali pa kazi kikamilifu.
“Tukitumia teknolojia kwa njia sahihi, salama, na jumuishi, tunaweza kuongeza tija kazini, kuboresha mazingira ya kazi, na kuhakikisha kila mtu anafaidika na maendeleo haya ya kidijitali,” amesema Mhe. Kikwete
Kadhalika, ametoa wito kwa wadau wa masuala ya kazi kuhakikisha wanaangalia mbinu bora za kutumia akili mnemba (AI) na teknolojia za kisasa ili kupunguza vihatarishi kwa wafanyakazi.
Akizungumza awali Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda amesema kuwa takwimu za usajili na ukaguzi katika kipindi cha miaka 3 kumekuwa na ongezeko la usajili kutoka 4,226 hadi 12,540 hali inayoashiria kwamba waajiri wanatambua umuhimu wa kusimika mifumo ya afya na usalama mahali pa kazi ili kulinda wafanyakazi.
Mwakilishi mkazi wa Kanda ya Afrika Mashariki wa Shirika la Kazi (ILO) Bi. Caroline Mugalla amesema matumizi ya Akili Mnemba (AI) na teknolojia ya kidigitali kwa asilimia kubwa yanapunguza visa vya ajali na magonjwa mahali pa kazi. Pia ameeleza kuwa kuna vihatarishi kama vile kupoteza baadhi ya kazi kutokana na matumizi hayo ya teknolojia.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Bi. Suzanne Ndomba amesema waajiri nchini wameendelea kutumia mifumo na teknolojia za kidigitali kuboresha ufanisi, kupunguza muda wa uzalishaji ili kuongeza tija sambamba na kulinda afya na usalama wa wafanyakazi wao.
Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA), Tumaini Nyamhokya, amesema wafanyakazi wanatambua mabadiliko yanayoletwa na uwepo wa teknolojia ya kisasa, ila wanashauri mabadiliko hayo yasiathiri uwepo wao na shughuli wanazozitekeleza sehemu za kazi.