News
Naibu Waziri Kisuo afungua mafunzo ya ajali za kikazi kwa Madaktari
Madaktari 1,894 kutoka Mikoa sita ya Tanzania bara wamepatiwa mafunzo maalum ya kuwaongeza uelewa na ujuzi katika kushughulikia masuala ya ajali za kikazi na magonjwa yatokanayo na kazi.
Aidha, Mafunzo hayo yamelenga kuimarisha utoaji wa huduma kwa wanufaika wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF).
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mafunzo hayo leo Disemba 15, 2025 Mkoani Tanga, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Rahma Kisuo, amesema Serikali imeendelea kuwekeza katika mafunzo ya rasilimali watu ili kuhakikisha wafanyakazi wanaopata ajali au magonjwa ya kikazi wanapata huduma stahiki kwa wakati na kwa viwango vinavyokubalika kitaaluma.
*“Hadi sasa jumla ya Madaktari 1,894 wamepatiwa mafunzo ya awali ya jumla kwa madaktari (general medical practitioners training), huku madaktari 217 wakishapatiwa mafunzo ya vitendo ya kufanya tathmini ya athari za ulemavu (hands-on impairment assessment training)”* amesema.
Mhe. Kisuo ameongeza kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwajengea madaktari uelewa wa taratibu za kuwahudumia wanufaika wa WCF, kuwawezesha kufanya tathmini sahihi ya athari za kibaiolojia zinazotokana na ajali za kikazi au magonjwa yatokanayo pamoja na kuwajengea uwezo wa kutambua magonjwa yatokanayo na kazi.
Awali akizungumza Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma, amesema Mafunzo yameandaliwa na WCF kama kuuwezesha Mfuko kutekeleza vyema jukumu la kutoa huduma za matibabu kwa wanufaika na kufanya tathmini sahihi na kwa wakati pindi mfanyakazi anapoumia au kuugua kutokana na kazi.
Vile vile, Dkt. Mduma amebainisha kuwa mafunzo hayo yamewakutanisha pamoja madaktari kutoka hospitali za umma na binafsi, kuanzia ngazi ya vituo vya afya hadi hospitali za rufaa za kanda, hususan kutoka Kanda ya Kaskazini, jambo litakalosaidia kubadilishana uzoefu na kuimarisha ushirikiano katika utoaji wa huduma bora kwa wanufaika wa WCF.
Naye, Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo Dkt. Salma Nassor amesema mafunzo hayo yanasaidia kuwaweka pamoja, kubadilishana uzoefu na kuimarisha ushirikiano katika utoaji wa huduma bora kwa wanufaika wa WCF.
