News
Watu wenye Ulemavu wahimizwa kuchangamkia fursa
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye ulemavu Zuhura Yunus, ametoa wito kwa Watu wenye Ulemavu kuchangamkia fursa ya Mafunzo ya mbinu bora za Kilimo, Elimu ya Fedha, Masoko na Ujasirimali ili waweze kukua kiuchumi.
Amebainisha hayo Aprili 25, 2025 Mkoani Singida alipotembelea wanufaika wa mradi wa mafunzo hayo yanayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Sightsavers, Chama cha Watu Wenye Ualbino Tanzania (TAS), Serengeti Breweries na Sustainable Agriculture Foundation.
Aidha, amesema mradi huo unatekelezwa katika Halmashauri mbili za Mkalama na Manispaa ya Singida ambapo amewataka wanufaika kutumia vyema fursa ya mafunzo hayo na kufikia malengo waliyokusudia ikiwemo kuajiriwa na kujiajiri wenyewe.
Vile vile, Naibu Katibu Mkuu, Zuhura Yunus ametembelea na kukagua Mashamba 4 ya mradi wa uwezeshaji Uchumi kwa Watu Wenye Ulemavu katika Kijiji cha Lukomo na Iguguno kata ya Iguguno Wilaya ya Mkalama Mkoani Singida.
Kadhalika, ameupongeza Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama kwa kuendelea kutoa elimu kwa wakulima kupitia Mashamba darasa ili kuwezesha kundi hilo la Watu wenye Ulemavu kupata tija katika kilimo chao.