News
Serikali yapandisha kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa umma
Serikali imepandisha kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa umma kwa asilimia 35.1 kwa lengo la kuimarisha ustawi kwa wafanyakazi.
Hayo yamebainishwa leo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani Kitaifa (Mei Mosi) mkoani Singida katika viwanja vya Bombadia.
Amesema kuwa maamuzi ya serikali kupandisha mishahara imesababishwa na kasi ya ukuaji wa Uchumi kupanda hadi kufikia 5.5% kwa mwaka, ambapo ukuaji huo umechangiwa na wafanyakazi kujituma na kufanya kazi kwa bidii.
Aidha, nyongeza ya mshahara itaanza kutumika mwezi Julai 2025 huku ngazi zingine za mshahara zikiendelea kupanda kwa viwango vizuri kadiri ya namna bajeti itakavyoruhusu.
Halikadhalika kwa upande wa wafanyakazi wa sekta binafsi Rais Dkt. Samia amesema bodi ya kima cha chini cha Mshahara inaendelea na tathmini kwa lengo la kuboresha viwango vya mishahara kwa sekta binafsi.
Vile vile Mhe. Rais Dkt. Samia ameeleza kuwa serikali itaendelea kushirikiana na wafanyakazi ikiwemo kuzifanyia kazi changamoto zinazowakabili.
Awali akizungumza Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa amesema jitihada kubwa zinazofanywa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha mazingira ya kazi nchini, kuongeza fursa za ajira pamoja na kuendeleza mazungumzo kati ya Serikali na vyama vya wafanyakazi zimeleta manufaa makubwa kwa wafanyakazi nchini.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Ridhiwani Kikwete amesema Wizara yake itaendelea kusimamia misingi ya UTATU katika kusimamia utekelezaji wa Sheria za Kazi ili kuimarisha viwango vya kazi kwa kuzingatia Sheria na Mikataba ya Kimataifa inavyoelekeza.