News
Naibu Katibu Mkuu Zuhura asisitizwa wafanyakazi kufanya mazoezi kuimarisha afya zao
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Zuhura Yunus amewataka watumishi walioshiriki bonanza lililoandaliwa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali Pa Kazi (OSHA) kujenga mazoea ya kufanya mazoezi mara kwa mara ili kulinda na kuimarisha afya zao.
Amebainisha hayo Aprili 26, 2025 wakati akifunga bonanza hilo lililofanyika katika viwanja vya VETA Singida ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya kimataifa kuelekea siku ya usalama na afya duniani ambayo kitaifa yanafanyika mkoani Singida.
Aidha, Naibu Katibu Mkuu Zuhura amesema serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kusisitiza umuhimu wa michezo na mazoezi kwa wananchi ili kuimarisha afya na kupambana na magonjwa yasiyoyakuambukiza.
“Mazoezi huimarisha afya ya akili na mwili na huepusha magonjwa hasa nyemelezi, hivyo mabonanza yanasaidia kuhamasisha wananchi kuwa na mwamko wa kufanya mazoezi,” amesema
Kadhalika, amepongeza OSHA kwa kushirikiana na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida kwa kuandaa bonanza hilo la michezo ambalo limewezesha washiriki kutoka maeneo mbalimbali kushiriki kwa wingi.
Naye Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda amesema bonanza hilo ni sehemu ya kampeni ya OSHA inayolenga kuhamasisha michezo kwenye maeneo ya kazi ili kuwezesha wafanyakazi kuondokana na vihatarishi ikiwemo magonjwa kama vile shinikizo la damu, kisukari na saratani ambayo yamekuwa kwa wingi katika maeneo ya kazi.