Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Bilioni 10.5 kutatua changamoto ya Ajira sekta ya Uvuvi - Katambi


Ili kukabiliana na changamoto ya ajira nchini, Serikali kupitia Wizara ya Uvuvi na Mifugo imetenga Shilingi bilioni 10.5 kwa ajili ya kuwezesha mitaji na miradi ya vijana.

Kauli hiyo imetolewa leo Mei 24, 2024 na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi kwenye hafla ya kufunga mafunzo kwa vitendo ya uvuvi na ukuzaji viumbe maji kupitia programu ya jenga kesho iliyo bora (BBT) iliyofanyika jijini Mwanza ambapo amesema fedha hizo zinatarajiwa kuwainua vijana na kuchangia katika pato la taifa kupitia sekta ya uvuvi na mifugo.

"Serikali kupitia wizara ya uvuvi na mifugo imetenga Sh10.5 bilioni kwa ajili ya mitaji na miradi ya vijana nchini hii ikiwa ni mwendelezo wa Serikali katika kuwainua kiuchumi vijana na kukabiliana na changamoto ya ajira nchini," amesema Katambi

Mbali na fedha hizo pia amewaasa vijana nchini kutengeneza vikundi na kuandika maandiko ya miradi ya kuomba mikopo ya asilimia 10 inayotarajiwa kuanza kutolewa tena katika Halmashauri zote nchini kuanzia Juni 2024.

Akiunga mkono hoja hiyo Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Profesa Riziki Shemdoe amesema baada ya mikopo hiyo kuanza kutolewa kijana mmoja atakuwa na uwezo wa kukopeshwa kuanzia Shilongi milioni 1 mpaka Shilingi milioni 50 huku kwa upande wa wenye vikundi ikiongezeka.

Akisoma risala ya wahitimu hao, Muhsin Mohamed kutoka Kagera amesema kupitia mafunzo hayo wamejifunza namna ya kutunza fedha, uundaji na usajili wa vikundi, uandishi wa maandiko ya miradi na jinsi ya kuendesha miradi hiyo huku yakiambatana na mafunzo kwa vitendo.

Katika hafla hiyo jumla ya vijana 291 kati ya 300 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar wamehitimu mafunzo ya muda mfupi yaliyoendeshwa kwa muda wa miezi mitatu tangu Februari 16 mwaka huu na kufungwa leo huku wengine tisa wakishindwa kutokana na sababu mbalimbali.