Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Serikali ya Awamu ya Sita inajivunia Ushirikiano wa Watumishi: Waziri Ridhiwani Kikwete


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Ridhiwani Kikwete ameipongeza Menejimenti na watumishi wa Ofisi hiyo kwa ushirikiano uliofanikisha Serikali ya Awamu ya Sita kupata mafanikio katika sekta za Kazi, Vijana, Ajira, Watu wenye Ulemavu na Kinga ya Jamii.

Amebainisha mafanikio hayo leo Agosti 21, 2025 wakati wa kikao cha pamoja na watumishi wa Ofisi hiyo kwa lengo la kuwashukuru watumishi na kuwapongeza kwa kutekeleza majukumu kwa ufanisi na tija katika kipindi chote alicho hudumu na kuiongoza Ofisi hiyo.

Amesema kuwa katika miaka minne ya Uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Ofisi hiyo imepata mafanikio makubwa ikiwemo kupunguza kodi ya mishahara kutoka asilimia 18 hadi 9, kutoa vibali 55,642 kwa wageni waliokuja kufanya kazi na kupunguza muda wa utoaji wa vibali vya kazi kutoka miezi miwili hadi siku 14.

Mafanikio mengine, ni kutoa mikopo nafuu kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana yenye thamani ya shilingi bilioni 3.2 kwa zaidi ya vijana 164,000, Serikali imezalisha ajira zaidi ya milioni 8 kupitia miradi ya Bomba la Mafuta, Reli ya Kisasa (SGR) na bwawa la Nyerere. Vilevile, Serikali imefanikiwa kupandisha pensheni ya chini kutoka shilingi 100,000 hadi 150,000 kwa mwezi.

Mhe. Ridhiwani aliendelea kusema mafanikio mengine ni watanzania 7,907 kupelekwa kwenye ajira nje ya nchi na kutoa mafunzo ya uanagenzi kwa vijana 121,526 katika sekta za kilimo, TEHAMA na ujenzi, ikiwemo mafunzo ya uzoefu wa kazi kwa vijana 22,176 kupitia utarajali.

Naye Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mary Maganga akizungumza kwenye kikao hicho alisema Ofisi hiyo imefanikiwa kuandaa nyaraka mahsusi za utendaji kazi ikiwemo Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya (2007), Toleo la mwaka 2024; Sera ya Taifa ya Kinga ya Jamii ya mwaka 2023 pamoja na mkakati wake;; Mpango kazi wa Taifa Haki na Ustawi kwa Watu Wenye Ualbino 2024/2025 – 2028/2029 (MTHUWWU); na Mpango maalum wa Vifaa Saidizi (NATS).