Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Mhe. Ridhiwani Kikwete azindua Miongozo na Mifumo ya Kielektroniki ya Ofisi ya Waziri Mkuu


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Ridhiwani Kikwete amezindua miongozo mitatu na mifumo ya kielektroniki miwili ambayo inalenga kuimarisha uratibu, usimamizi na uendeshaji wa masuala ya Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu.

Miongozo na Mifumo iliyozinduliwa ni pamoja na Mwongozo wa Majadiliano baina ya Serikali, Vyama vya Wafanyakazi na Vyama vya Waajiri wa Mwaka 2025, Mwongozo wa Uratibu wa Vyama vya Watu Wenye Ulemavu wa Mwaka 2025, Mwongozo wa Wakala Binafsi wa Ajira wa Mwaka 2025, Mfumo wa Kitaifa wa Kieletroniki wa Taarifa za Soko la Ajira wa Mwaka 2025 na Mfumo wa Kielektroniki wa Usimamizi wa Mashauri ya Usuluhishi na Uamuzi wa Mwaka 2025.

Akizindua leo 22 Agosti, 2025 jijini Dodoma, Mhe. Ridhiwani Kikwete amesema kuwa miongozo na mifumo itasaidia kujenga misingi ya majadiliano yenye tija na jumuishi, uimarishwaji wa haki za Watu wenye Ulemavu, usimamizi makini wa mawakala wa ajira, pamoja na uwepo wa mifumo ya kisasa ya kukusanya na kuchakata taarifa za soko la ajira, sambamba na kuendesha mashauri ya kazi na usuluhishi kwa ufanisi mkubwa kupitia mifumo hiyo ya kielektroniki.

Aidha, amesema miongozo na mifumo iliyozinduliwa inalenga kutokomeza umaskini na kuimarisha uwezo wa wananchi hususan wanawake, vijana, na Watu wenye Ulemavu ili waweze kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa.

Kadhalika, Waziri Ridhiwani Kikwete ameshukuru wadau kwa ushirikiano wao katika uandaaji wa miongozo na mifumo hiyo. Amesema mchango wa wadau hao itasaidia kufanikisha malengo yaliyopangwa katika kuhakikisha vijana, wafanyakazi, waajiri na Watu wenye Ulemavu wanapata fursa sawa na wanashiriki kikamilifu katika nyanja zote.

Kwa upande wake Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mary Maganga amesema kazi ya uandaaji wa miongozo na mifumo hiyo ilikuwa shirikishi ambapo wadau mbalimbali wa Maendeleo walishirikishwa ikiwemo Shirika la Kazi Duniani (ILO), Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), TPSF na TRAA.