Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Waziri Ridhiwani ahimiza wajibu wa Waajiri kuwalinda Wafanyakazi dhidi ya vihatarishi vipya vya matumizi ya Teknolojia


WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Mhe. Ridhiwani Kikwete, amesema matumizi ya teknolojia na akili mnemba (Artificial Intelligence) ni nyenzo yenye nguvu kubwa, hivyo waajiri wanapaswa kuhakikisha matumizi hayo yanaambatana na hatua madhubuti za kuwalinda wafanyakazi dhidi ya vihatarishi vipya kazini.

Mhe. Ridhiwani ametoa kauli hiyo leo jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelekea maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Usalama na Afya Mahali Pa Kazi Duniani, ambayo huadhimishwa kila mwaka tarehe 28 Aprili.

“Matumizi ya teknolojia na akili mnemba si adui yetu, bali ni nyenzo yenye nguvu kubwa. Kauli mbiu ya mwaka huu imelenga kuhamasisha na kuwakumbusha waajiri kuanza kujiandaa kutumia Akili Mnemba katika uzalishaji na utoaji wa huduma bora,” amesema Waziri.

Aidha, ameeleza kuwa teknolojia huongeza ufanisi katika kazi, lakini pia huibua changamoto mpya za kiusalama, hivyo ni muhimu kuambatana na mapitio ya kanuni za usalama, mafunzo sahihi na ufuatiliaji endelevu ili kuhakikisha mazingira salama na salama zaidi kwa wafanyakazi.

Waziri Ridhiwani pia amewahimiza waajiri wote nchini kuhakikisha wanasajili maeneo yao ya kazi kwa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), sambamba na kutekeleza matakwa ya Sheria Na. 5 ya mwaka 2003 kuhusu Usalama na Afya Mahali pa Kazi.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, amefafanua kuwa mwajiri yeyote anayebainika kukiuka sheria hiyo huchukuliwa hatua za kisheria kwa kuhatarisha usalama wa wafanyakazi wake. Aliongeza kuwa ni kosa la jinai kwa mwajiri kutosajili eneo la kazi kwa OSHA, kwani hilo linaweka maisha ya wafanyakazi hatarini.

Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu, inasema "Nafasi ya Akili Mnemba na Teknolojia za Kidijitali katika Mapinduzi ya Usalama na Afya Kazini", ikiwa ni wito kwa nchi wanachama kutumia teknolojia kwa namna salama na jumuishi kwa wafanyakazi wote.