News
Waziri Kikwete ataja Mikakati ya Serikali kuimarisha huduma kwa Watu Wenye Ulemavu
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Ridhiwani Kikwete amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuhakikisha Watu wenye Ulemavu wanapata fursa ya kushiriki kwenye shughuli kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Aidha, amesema jitihada hizo ni pamoja kutoa vifaa saidizi kwa kundi hilo sambamba na kuendelea kuboresha miundombinu katika maeneo ya utoaji wa huduma ya Elimu, Afya na TEHAMA ili kuhakikisha inakuwa rafiki na fikivu.
Mhe. Kikwete amebainisha hayo leo Aprili 13, 2025 Jijini Dar es salaam wakati aliposhiriki katika mbio maalum za 'Run for sight Marathon 2025' zilizoandaliwa na Lions Club International – Tanzania.
Amesema kuwa mbio hizo zinalenga kuhamasisha wadau mbalimbali kuchangia rasilimali zitakazowezesha upatikanaji wa vifaa na huduma kwa Watu wenye Ulemavu hususan wanaokabiliwa na changamoto ya uoni hafifu.
“Ni matumaini yangu kuwa fedha zitakazokusanywa zitachangia kwa kiasi kikubwa kutatua changamoto ya uoni hapa nchini, hivyo kuhakikisha watu wenye Ulemavu wa kuona wanapata fursa za maendeleo na wanaweza kuchangia kwa ufanisi katika uchumi wa nchi.” amesema.
Vile vile, amesema Serikali kwa kushirikiana na Shirikisho la Watu wenye Ulemavu (SHIVYAWATA) wameendelea kuratibu na kufanya maadhimisho ya kimataifa ya Watu wenye Ulemavu hususan wasioona ikiwemo Maadhimisho ya Fimbo Nyeupe na Breille.