News
Serikali imeendelea kuboresha huduma kwa Watu wenye Ulemavu
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa amesema Serikali imeendelea kuboresha huduma kwa Watu wenye Ulemavu nchini ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii, kisiasa na kiuchumi.
Mhe. Majaliwa ameyasema hayo leo Aprili 9, 2025 Bungeni Jijini Dodoma wakati akiwasilisha hotuba kuhusu mapitio na mwelekeo wa kazi wa kazi za Serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026.
“Katika mwaka 2025/2026, Serikali itaendelea kuratibu utoaji wa huduma kwa Watu Wenye Ulemavu kwa kutekeleza Sera, Sheria, mikakati na mipango mbalimbali ya kitaifa, kikanda na kimataifa ili kuwawezesha Watu Wenye Ulemavu kiuchumi, kijamii na kisiasa kwa kuimarisha ushiriki wao katika nyanja zote,” amesema
Aidha, Mhe. Kassim Majaliwa amebainisha kuwa Serikali imezindua Mpango kazi wa Taifa wa Ustawi na Haki kwa Watu Wenye Ualbino kwa Mwaka 2024/2025 – 2028/2029 ambao umeainisha hatua zinazohitajika katika kuzuia, kukabiliana na kutokomeza ukatili kwa Watu Wenye Ualbino.
Vile vile, amesema Serikali ilizindua Mkakati wa Taifa wa Teknolojia Saidizi 2024 – 2027 ambao unatoa mwongozo wa kimkakati kwa sekta zote kuweka mazingira wezeshi ili kila mwenye uhitaji wa teknolojia saidizi aweze kupata kwa wakati na kwa gharama nafuu.
Pia, Mhe. Majaliwa amesema Serikali imezindua kanzidata na Mfumo wa Taarifa za Watu Wenye Ulemavu unaotokana na matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 ambapo matumizi ya Takwimu ya Sensa zitawezesha kutayarisha programu za kuwajengea uwezo Watu Wenye Ulemavu kutumia fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali na wadau wa maendeleo ili kujiendeleza kiuchumi, kijamii na kimazingira.