News
Serikali imedhamiria kujenga Taifa linalozingatia usawa wa Kijinsia kwa Vijana - Kikwete
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Mhe.Ridhiwani Kikwete amesema Serikali imedhamiria kuwezesha vijana kuwa mstari wa mbele katika kujenga Taifa linalozingatia usawa wa kijinsia kwa vijana wa kiume na kike.
Mhe.Ridhiwani ameyasema hayo Aprili 17, 2025 katika mkutano mkuu wa viongozi wa Idara ya Vijana wa Kampeni ya Kitaifa ya Kupinga Ukatili wa Kijinsia na Ukatili kwa Watoto nchini Tanzania (SMAUJATA) jijini Tanga.
Amesema vijana ni rasilimali muhimu sana kwa maendeleo ya Taifa na kwamba wanapaswa kusimama imara katika kutetea misingi ya haki, ukweli, uwajibikaji na mshikamano wa kitaifa.
“Vijana mnapaswa kujitambua kama sehemu ya suluhisho si tatizo katika changamoto zinazoikabili jamii yenu na nchi kwa ujumla, kujitambua huku kunahitaji maarifa, maadili, moyo wa kujituma, na bidii isiyotetereka"
Mhe.Waziri Ridhiwani amesema Taifa linawahitaji wakiwa na ari, hamasa na moyo wa kujitoa kwa dhati katika kila sekta ya maisha kuanzia elimu, kilimo, afya, teknolojia, biashara, uongozi na utumishi wa umma
Vile vile, Serikali inaeendela kufanya juhudi mbalimbali Kwa Ustawi wa Vijana ikiwemo uzinduzi wa sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana toleo la Mwaka 2024 yenye hoja kumi na tatu za kisera inayowezesha jamii yote kuwa mstari wa mbele kutetea masuala ya vijana na jinsia.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Japhari Kubecha akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Tanga Dkt. Batilda Buriani amesema wataendelea kushirikiana na makundi yote ya kijamii katika kupambana na ukatili wa kijinsia na kuhakikisha vijana wanapata kwa wakati mikopo inayotolewa na halmashauri ili wafanye shughuli za uzalishaji na kujikwamua kiuchumi.
Awali, Mwenyekiti wa SMAUJATA Taifa, Sospeter Bulugu, amesema kuna haja ya kuzungumza na vijana kupitia njia mbalimbali ili kufahamu umuhimu wa taarifa sahihi katika umri wao wa ujana na kutambua fursa zinazowazunguka.